NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI NA MBILI(22)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


“Karibuni,”alisema nesi aliyekuwa mapokezi baada ya kuona sura za wateja hao walionekana ni watu wanaonukianukia hela.
“Dokta Malienge yupo?” aliuliza Suzy yule nesi aliitikia na kutoka kisha akawapeleka chumba alichomo yule daktari.
“shikamoo dokta,” alisalimia kwa uoga kidogo Jackline hasa baada ya kugundua Daktari mwenyewe ni mtu mzima.
“marahaba,” alijibu Daktari huyo bila kuangalia wanaomsalimia kwa kuwa alionekana bize akiwa anaandikaandika vitu huku akiwa amekaa kwenye kiti.
Chumba hicho kilikuwa kikubwa ambapo kilikuwa kimegawanyika katika sehemu mbili. Kuna sehemu ambayo imetengwa kwa mapazia na kila upepo ulipopuliza kulionekana kuna kitanda na mikasimikasi mingi juu ya kisinia kidogo cha pembe nne.
Mazingira hayo yalianza kumtia uoga Jackline akatamani aghairi lakini uzito wa penzi lake kwa Peter ukamfanya aendelee na kusudio lake la kutoa mimba.
“enhee nani mgonjwa?” aliuliza yule daktari baada ya kuinua kichwa chake na kuwaona warembo wawili wakiwa wameketi pembeni yake.
“Dokta, huyu ndugu yangu hapo alipo ana ujauzito na kuna mtu anataka kumuoa hivyo anataka kuutoa maana kama huyo bwana ake akigundua kama ana mimba halafu siyo yake, ndoa tutaisikia kwenye bomba tu,” alitunga uongo Suzy.
“Haahaa! Kwa hiyo ni kwa ajili ya ndoa? Ok, haina shida hapa kila kitu kitaisha,” aliongea Dr. Malienge lakini ghafla alishangaa kibangili chake cha mkononi kikianza kumbana, akajua moja kwa moja lazima watu hao watakuwa na mkosi kwenye kazi yake.
Dk.Malienge akakumbuka masharti ya mganga kuwa pindi bangili hiyo ikimbana basi anatakiwa kuacha alichokuwa akikifanya mara moja kwa kuwa kuna jambo baya litampata.
Lakini kwa kuwa tangu aanze kufanya kazi akiwa na bangili hiyo ya miujiza hakuwahi kubanwa nayo, akadharau kwa tamaa ya fedha. Akamwangalia Jackline na kumtaka amuoneshe kadi yake ya mahudhurio ya kliniki.
Baada ya kuangalia kwa makini ile kadi akamtahadharisha Jackline kuhusu madhara ya kutoa mimba hiyo ambayo ilikuwa imeshatimiza miezi minne sasa, kisha akamtajia gharama zake ambazo ni shilingi laki moja na kumuelekeza kwa kulala wakati akisubiri vifaa vya kuchoropoa mimba vikiwa vinaandaliwa.
Wakati wote Dk. Malienge alipokuwa akiandaa vifaa hivyo kwa kuvichemsha, akawa bado na wasiwasi, akahisi pengine bangili hiyo inambana kwa ishara pengine Jackline atamfia baada ya kumtoa mimba, lakini akapuuza hofu hiyo kwa kujiapiza atakuwa makini. 
Akawaza pengine ni mtego wa polisi kuja kumkamata, lakini akadharau pia kwa sababu anajulikana na polisi wa Manzese nzima. Bado swali lilikuwa tatizo ni nini?
Tamaa ikaishinda nafsi, Dokta Malienge aliingia kwenye kile chumba alichomo Jackline na sindano yake ya ganzi akamchoma nayo Jackline kwa ajili ya kumuondolea maumivu wakati wa kumtoa mimba kisha akavaa glovuzi zake taratibu huku akiwa na kisinia cha mikasi ya kutolea mimba na koleo la kuchoropolea.
Kwa mtazamo wa vifaa hivyo, unaweza kuhisi maumivu makali ya tumbo hata kama hautoi mimba wewe, lakini ndiyo hali halisi na Jackline alikuwa tayari kupitia hatua hiyo akiamini mimba hiyo ni kikwazo kwenye penzi lake na Peter.
Wakati Daktari akiwa tayari akiwa ameshajiandaa mara kukasikia mlio mkali wa mbwa nje ya dirisha la chumba alichomo, kila mmoja akashtuka. Kwa hofu Dokta Malienge alirudisha vifaa vyake na kuvificha kwenye kabati kisha akafunga kwa ufunguo na haraka kwenda kwenye mlango wake akijifungia kwa ndani yeye na Jackline kwa woga.
Jackline aliyekuwa amekolea sindano za ganzi alijikuta hawezi hata kunyanyua miguu yake, akaishia kuhema tu kwa hofu. Suzy aliyekuwa ameketi kwenye benchi la varanda nje ya chumba cha daktari alisikia sauti hiyo akahisi anaijua. Akiwa katika mawazo hayo, kufumba na kufumbua alishangaa kuona Simba akiwa miguuni pake, akamng’ata mguu wake na kumnyofoa kipande cha nyama jambo lililowafanya wagonjwa wengine waliofika kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya matibabu kila mmoja atafute pa kukimbilia.
Makelele ya Suzy na wagonjwa wengine ndiyo yalimshtua Dk Malienge ambaye alijua huenda kuna tatizo kubwa zaidi, akafungua mlango na kutoka nje.
Hakuona chochote cha maana zaidi ya kusikia stori za mbwa mkubwa mweusi aliyewavamia na kukimbilia nje, Dokta Malienge, akajua haraka kuwa, hiyo ni hatari iliyoifanya ile bangili yake kumbana. 
Lakini cha kushangaza iliendelea kumbana kuashiria hatari nyingine akaona kama mbwai na iwe mbwai hawezi kuendelea kutoa mimba ya Jackline. 
Kwa harakaharaka akachukua vifaa vya huduma ya kwanza na kumfunga bandeji Suzy na madawa kadhaa na kuwataka mara moja waondoke kwenye zahanati yake .
Wakiwa hawaelewi kilichotokea Suzy akambeba Jackline ambaye miguu yake ilikuwa mizito kwa ganzi na kupanda bajaji wakirudi nyumbani kwao kila mmoja akiuguza maumivu yake bila kuongeleshana.

ITAEDELEA JUMANNE
Post a Comment
Powered by Blogger.