NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA ISHIRINI(20)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Wakiwa wanaanza kujivinjari, mara Peter akashtuka na kuinua uso wake, akihisi kuna kitu amekisikia;
“Nini mbona upo hivyo, endelea bwana,” alilalama Suzy kwa sauti ya puani akionekana kuelemewa na tomasatomasa za Peter.
“Nimesikia kitu,” alisema Peter huku akiacha kufanya alichokuwa akikifanya na kusikilizia kwa makini zaidi.
“Hamna chochote, hofu yako tu,” alisema Suzy huku akijivirigaviriga kama nyoka pale kitandani.
Wakati huo Jackline aligundua kukurukakala kwenye chumba cha Suzy akatembea kuelekea huko na kugundua mlango ulikuwa wazi, akafungua na kushangaa kumuona Suzy akiwa anakukuruka pale kitandani huku shuka likiwa limestiri kuanzia kiunoni hadi miguuni tu na kumuacha wazi sehemu za matiti yake.
Peter naye huku kijasho kikiwa kinamtoka akiwa na shuka lake kiunoni alimshikilia kwa mikono yake yenye nguvu Suzy na kumkandamiza kwa nguvu pale kitandani akijifanya kama vile anamzuia kwa jambo fulani.
“Jacky njoo haraka unisaidie!” aliongea Peter baada ya kumuona Jackline amesimama mlangoni akiwa ameduwaa asijue nini kinachoendelea.
“kwani kuna nini mbona mpo hivyo!” aliuliza Jackline akiwa bado hajaelewa mazingira hayo ya kaka mtu na shuka kiunoni na dada yake nusu utupu wakiwa chumbani usiku.
“Amepandisha mashetani, hebu njoo nisaidie kumshikilia asije akakimbilia nje!” aliendelea kupiga makelele Peter.
“mashetani!” alishangaa Jackline lakini akakimbilia kutoa msaada na kumsaidia kumshikilia Suzy pale kitandani.
Peter akiwa katika kiwango chake cha maigizo, akapaza sauti akijifanya anasali na kukemea mapepo kama wafanyavyo Walokole tena kwa sauti ya juu baada ya dakika chache mara Suzy akaacha fujo zake na kutulia tuli.
“Peter kuna nini kinaendelea?” aliuliza Jackline huku akionekana bado hajaelewa nini kinachoendelea.
“Huelewi nini sasa! We unaona kabisa Suzy amepandisha mashetani, tena nashukuru Mungu nilishtuka mapema niliposikia akipiga makelele maana alikuwa anataka kukimbilia nje.
“Nikahangaika naye, hadi kumrudisha ndani na kumsitiri, maana ana majini mabaya kweli huyu. Uzuri mimi mwenyewe nina upako ndiyo maana nilipoyakemea mara moja yameondoka,” alisema Peter macho yake yakiwa makavu.
“He! Kumbe Suzy ana mashetani, nilikuwa tayari nimeshaanza kuwahisi vibaya!” aliongea Jackline.
“We! mdogo wangu namjua, kwani hajawahi kukupandishia hapa nyumbani?”
“mh! Tangu nimjue sijawahi kumuona amepandisha, haya mauzauza ndiyo nayaona leo, sasa ndiyo utanifanya nimuogope kweli yaani!”
“hata hivyo hana matatizo, mpaka apandishe, basi lazima kuna kitu kibaya kimetokea tena kwa mwaka mara moja, mashetani yake hayamjii hovyohovyo,” aliongea Peter akimpoza moyo Jackline.
“mh haya bwana lakini kwa hali hii, bora uwe unakaa hapa na sisi ili yakitokea haya mauzauza umalizane nayo wewe mwenyewe,” alisema Jackline wakati huo Suzy akajigeuza pale kitandani na kufumbua macho akauliza kwa sauti ya kichovu akijifanya haelewi moja wala tatu; “Nyie vipi? Kwani kuna nini kimetokea?”
Basi hapo Jackline akadandia na kuanza kumuelezea jinsi alivyopandisha mashetani na kudai alikuwa na nguvu mno kiasi cha kuwashinda. Tena akamsifia Peter kwa jinsi alivyomuombea kwa ujasiri na kuyakimbiza mapepo yote.
Wakati huo wenyewe wakakonyezana na kujiongelea moyoni; “hili bwege kweli.”
Baada ya maongezi mafupi, Jackline alimbeba bwana ake kisha wote wakaingia kujifungia chumbani kwao kumalizia kipande cha usiku kilichobakia.
Huko nyuma Suzy akashusha pumzi akimsifia jinsi Peter alivyokuwa na akili sana kiasi cha kufikiria uongo ule uliotukuka. Akaapa kuanzia siku hiyo hataendekeza kung’ang’ania jambo ambalo Peter anamkataza maana aliona utajiri ukiwa hatiani kupotea mikononi mwao siku hiyo ikiwa Jackline angewafumania.
“Mpenzi, mimi nimeona kesho ndiyo tuende kwa daktari tukaitoe hii mimba na siyo wiki ijayo tena. Maana naona kama vile sitakutendea haki!” alisema Jackline akimwambia Peter.
“usiseme hivyo Jacky, wewe fanya chochote unachoamua sikulazimishi ufanye kitu ambacho haukitaki,”
“ndiyo nimeshaamua hivyo,” “sawa, nipo pamoja na wewe maana ninatamani sana tusiishie hivi, nataka nikuoe tena muda mfupi tu kuanzia sasa,” alifunguka Peter akijua fika ikiwa atamuoa Jackline basi atapata haki ya kuzisimamia mali za Tinonko.
“hilo nalifikiria usijali,” alibonga Jackline akiwa ametulizwa kifuani kwa mwanaume.
***
Ndani ya chumba kidogo chenye giza ndipo Tinonko alishtukia kutoka kwenye usingizi mzito aliolala, akakagua na kugundua hakukuwa na kitu chochote zaidi ya kitanda kidogo.
Kibaya zaidi aligundua amefungwa kwa pingu kwenye kona ya kile kitanda miguu na mikono. AKiwa anarudisha kumbukumbu kujua nini kilichotokea hadi akafika hapo, mara akasikia vishindo vya watu wasiopungua watatu. Hatua zao zilifika hadi nje ya mlango wa chumba alichomo na kufunguliwa.
Cha ajabu watu walioingia walikuwa wote wamejifunga sura zao kama maninja, tena wakiwa na begi la zana mbalimbali zenye ncha kuanzia kisu mpaka nyundo. Tinonko akajua moja kwa moja watu hao walikuwa ni kikosi maalumu cha jeshi cha kutesa mtu kwa ajili ya kupata taarifa.
Akahisi pengine hawakuwa wanamjua yeye ni nani basi akapiga kelele akisema; “mimi ni Kapteni Tinonko! Mwanajeshi namba 07832!”
Moja wa wale watu akajibu kwa dharau, “Tunajua,” kisha akatoa kisu kidogo na kumchoma nacho ubavuni.

ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.