NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI NA TISA(19)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Tinonko akafumbua macho taratibu kuangalia maajabu ya Mbirikimo ikiwa kweli waliyosema yametimia au lah! Japo kuwa ilikuwa ni giza sana kutokana na yeye kuanza safari yake jioni na kufika usiku, alifumbua macho na kugundua kuwa kweli alikuwa ametokea sehemu aliyokuwa akiitaka.
Ilikuwa ni katikati ya makao makuu ya jeshi la Tanzania, Ngome. Sehemu ambayo yote yalianzia hapo. Akashangaa jinsi alivyoweza kutumia muda mchache sana kuingia jijini kwa teknolojia ya kiajabu. Akafurahi na kupiga magoti kisha akabusu ardhi ya katikati ya miguu yake kwa mapenzi makubwa juu ya nchi yake.
Akiwa na sare zake za jeshi zilizochafuka mno huku akifichwa na giza la usiku akatembea kuelekea kwenye moja ya ofisi za Luteni au mkubwa yeyote anayemjua kambini hapo. Hata hivyo hakujua kama anaweza kukutana na mtu yoyote kwa usiku huo kwa kuwa wengi walikuwa wameshaenda makwao au walikuwa wamelala, ukiachilia vikosi vichache vya doria na wanajeshi wa mafunzo.
Taratibu akasonga akifuata ofisi ambayo inaonekana ikiwaka taa kwa ndani. Akiwa anataka kukunja kona akasikia ukelele nyuma yake.
“Chini ya ulinzi! Weka kila kitu chini! Songa hatua tano mbele!” alisema mtu huyo, kwa kuepusha hatari, Tinonko akatekeleza yale aliyoambiwa, ikiwemo kuweka silaha zake chini bila kusahau hata kile kikalabashi chake cha madini ya ruby, almasi na topaz za bluu, zote zenye thamani ya matrilioni ya Kitanzania.
Yule mwanajeshi aliyeonekana ni mlinzi wa eneo lile akapuliza filimbi, akatokea mwanajeshi mwingine nyuma yake. Wakaanza kukagua vile vitu huku wakionekana kushangaa mno.
“Nyuma geuka!” aliongea yule mwanajeshi kwa woga huku bunduki zao wote wawili wakiwa wamemuelekeza Tinonko. Wakamtazama Tinonko aliyegeuka taratibu huku ameshusha mikono na kuonekana nyota zake za begani na nishani zake za ushujaa ziking’ara kifuani mwake.
Kwa kuona hivyo wale wanajeshi ambao waligundua kuwa wamekosea kwa kumuamuru bosi wako kicheo, walikakamaa kama wamepigwa shoti kisha wakapiga saluti kiheshima huku wakiomba msamaha kama watoto wadogo.
Tinonko akatabasamu kisha akapiga hatua na kuinama akichukua zile silaha zake na kalabashi lake la madini. Kabla hajainuka alisikia mlio mwembamba wa bastola iliyofungwa kifaa cha kudhibiti sauti ‘Silensa’ ukiashiria risasi zimepita hewani.
Wanasema ukisikia “Shaa! ujue imekupata”, wale wanajeshi wawili walianguka chini kama mizigo ya lumbesa, wakati huo Tinonko alikuwa amechelewa mno akaona macho yake yakizidi kupoteza nguvu ya kuona wala miguu yake kusimama naye akadondoka chini kama kuti kavu.
Taswira ya mtu aliyevalia mavazi ya kijeshi na kufichwa na kiza usoni, ndiyo iliyoganda kichwani mwake. Mtu huyu ndiye aliyeonekana kwenye tivii za asili za Mbirikimo zilizokata mawasiliano mara tu alipoonekana.
Ni sababu ya mtu huyu ndiyo iliyofanya Aka-Baka amuonye Tinonko asirudi Tanzania hadi amjue adui yake vizuri, lakini yeye aling’ang’ania. 
Mtu huyo ndiye leo anampiga risasi Tinonko akiwa ndiyo kwanza amerejea kimaajabu Tanzania. Inavyoonekana ni wazi kwamba alikuwa amejipanga kwa shambulizi hilo; swali ni Je, alijuaje kama Tinonko angerudi usiku huo na kutua kambini hapo? au yale maneno ya Aka-Baka kuwa mtu huyo anaonekana kujua teknolojia za Mbirikimo ni ya kweli?
Eee Mungu muokoe Tinonko!

Usiku Jackline akiwa amelala aliota ndoto; Ndani ya ndoto hiyo alimuona mumewe Kapteni Tinonko akiwa anahangaika kuzuia moto uliokuwa ukiwaka ndani ya nyumba moja ambayo ndani yake Jackline alijiona tena akiwa na mtoto mchanga.
Katika kuhangaika huko, Tinonko alifanikiwa kumuokoa mtoto lakini Jackline mwenyewe ambaye cha ajabu hakuwa akisikia maumivu ya ule moto, alikuwa aking’angania kubakia ndani ya nyumba ile inayoungua.
Ghafla alisikia sauti ya mbwa inalia huko nje, akashtushwa kutoka kwenye ndoto ile ya kutisha na kujitazama huko na huku akihakikisha kuwa hajaungua kweli kama alivyodhania.
Akashusha pumzi na kutazama pembeni yake alipolala Peter, kwa mshangao wake hakumuona, akahisi huenda alikuwa chooni lakini kwa kuwa chumba hicho kina choo humohumo ndani aliinuka na kwenda kumtazama lakini hakumuona.
“Atakuwa ameenda wapi usiku huu!” aliwaza Jackline na kufungua mlango wa chumba chake akitoka nje kumuangalia Peter upande wa sebuleni, akidhania labda atakuwa amebanwa na kiu na kwenda kunywa maji au juisi.
***
Kwa upande mwingine alionekana Suzy akiwa ameketi kitandani kwake na Peter akiwa kama alivyozaliwa. Kuna kitu kilionekana kimefanyika au kitafanyika baina ya wapenzi hao wawili wanaojifanya mtu na kaka yake.
Peter akiwa amejifunga shuka tu kiunoni mwake na Suzy alikuwa akilivuta na kumuandama Peter aliyeonekana akitaka mchezo huo wa hatari uishe mara moja.
“Sikia Suzy! Hapa unafikiri Jacky akija na kutukuta hivi itakuwaje si atatushtukia!”
“Hana lolote, jana alikunywa sana, hapo mwenzako kalala fofofo, wewe nipe tu kidogo nikate hamu bwana, we unafikiri vizuri ulivyofanya na huyo Jacky wakati unaniacha nikiwa naona kila kitu,” alilalama Suzy kiasi cha kutoa machozi na kumfanya Peter amuonee huruma.


Post a Comment
Powered by Blogger.