NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI NA NANE(18)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Wakati akiendelea kumalizia maelezo yake mara akagundua jua ndiyo lilikuwa likizama, ndipo Tinonko akamgeukia Aka-Baka na kumkumbusha kuhusu kurudi nyumbani mara moja kama alivyoahidiwa kuwa ni jioni ya siku hiyo.
Basi kila mmoja akajipanga na zikachorwa alama za ajabuajabu pale ardhini kwa kutumia mavumba ya ngala za magharibi, kisha Aka-Baka akiwa na kuku wawili weupe akawachinja na kunyunyizia kumzunguka Tinonko; tena akasambaza manyoya yake kila upande kisha akamwambia Tinonko afumbe macho yake na kuvuta picha ya sehemu anayotaka kwenda bila kufumbua.
Akamuonya kuwa kabla ya kufanya jambo hilo kuwa ahakikishe kuwa hatafumbua jicho lake hata kwa dakika kwa kuwa endapo akifumbua wakati bado hajafika anapotakiwa kwenda basi kuna hatari ya kujikuta ameangukia katikati ya ulimwengu mwingine, sehemu ambayo haifai hata kidogo.
Naye Tinonko akahoji dalili gani zitamfanya ajue kama amefika au lah! Naye Aka-Baka akamwambia utasikia mtu akikufinya juu ya mkono wako wa kulia.
Baada ya kuambiwa hayo, Tinonko alilishikilia ndindindi lile kalabashi lake la madini mbalimbali alilopewa kama tunu kutoka kwa mbirikimo hao kwa kazi aliyowafanyia na hata yule mtoto wa maajabu mwenyewe ndiye aliyembariki na kumtakia safari njema.
Tinonko akafumba macho na kuvuta picha ya sehemu anapopataka, vumbi likatimka kuzunguka pale aliposimama akatamani kufumbua macho, lakini akayatilia maanani yale maneno ya Aka-Baka na kufumba macho nga nganga.


Nyumbani kwa Jackline kila kitu kilikuwa kimebadilika, hata mgeni angeingia siku hiyo angejua pengine kuna ugeni wa mtu fulani muhimu sana katika familia hiyo. Kumbe wapi zaidi ya Peter aliyekuwa akila na kujilamba mali za mwanajeshi.
Basi wakiwa wameshafanya yao na Jackline akanogewa akawa anamlazimisha Peter aghairi kuondoka na kulala siku hiyo. Lakini Peter kama vile machale yalikuwa yakimcheza siku hiyo akawa anafanya visingizio vya kutaka kuondoka.
Katika hali hiyo Jackline akatumia utundu wake, akamshika hapa mara pale na hatimaye akawasha swichi tena, mara wakagalagazana upya kama vile wao ndio walikuwa wameonana siku hiyo.
Wakaja kushtuka tayari ni majira ya saa nne usiku. Peter akasisitiza kuondoka kuliko kawaida na mwishowe akatumia nguvu na kuvaa nguo zake na kutoka hadi sebuleni ambapo alivaana uso kwa uso na Suzy akiwa amechukia kwelikweli.
Peter akamtazama Suzy na kuonesha ishara atulie, wakati huo Jackline akiwa na shuka tu mabegani, naye akatokeza na kujibaraguza mbele ya Suzy.
“Kaka yako anan’gang’ania kweli kuondoka basi ndiyo hivyo tena, nyie ndugu aganeni basi,” alisema Jackline.
“haya kaka kwaheri,” alisema Suzy na kumkumbatia Peter kiuongouongo.
Wakamfungulia mlango wa sebuleni na tayari Peter alikuwa ameanza kupiga hatua kuelekea lilipo geti huku akitathini thamani ya jengo hilo la kifahari na kugundua kuwa thamani yake inaweza ikavuka hata milioni 100.
Akatazama gari za thamani kama vile Land Rover na Cruiser zilizoegeshwa bila mwenyewe kuwepo zikiwa mpya na nzima kabisa.
Alipotaka kwenda mbali zaidi alishtukia akivamiwa na mbwa mkubwa nyuma yake ambaye alimlarua kwa hasira, kiasi cha mtu mzima kuanza kupiga makelele na kukimbilia ndani alipotoka akihema mno.

“Hahaaa mwanaume mzima muoga hivyo!” walicheka wakina Jackline baada ya kugundua Simba ndiye aliyemtimua Peter huko nje.
“Acheni masihara nyinyi huyu mbwa siyo wa kawaida! Hawezi kutoka huko na kunivamia mimi kiasi kile!” alilalamika Peter.
Basi ikabidi Jackline afungue mlango na kumsindikiza Peter hadi pale getini, lakini wakiwa wamepiga hatua chache tu kufikia lengo lao, mbwa huyo alirudi kwa kasi zaidi ya mwanzo tena akiwa amewaka hasira kiasi cha Peter aliyejificha nyuma ya Jackline kutimua mbio na kurudi ndani akimuacha Jackline peke yake pale nje akishangaa kilichomsibu mbwa huyo.
“Inawezekana hataki uondoke!” alisema Jackline baada ya kurudi ndani akimuangalia Peter aliyekuwa akihema kwa hofu.
“Acha masihara Jackline, mimi nataka kuondoka sasa hivi!” alisisitiza Peter.
“Si umeona hali ilivyokuwa huko nje! Hapa kuna mawili cha kwanza usubiri hadi asubuhi ifike arudishwe bandani, au umwambie dada ako Suzy akusindikize,”
“Akaaa! nani huyo mbwa mimi ndiyo hanipendi hata kidogo,” alijibu Suzy japo kuwa hakutaka Peter abakie pale hata kidogo maana wivu ulimuua.
Peter akaonekana hana cha kufanya zaidi ya kukubali kulala siku hiyo kwa Jackline.
Basi Jackline kimoyomoyo akamshuru Simba kwa kumfanya Peter abaki ndani bila kujua huenda mbwa huyo alinusa ujio wa bwana wake; Tinonko na kutaka awafumanie wakiwa humohumo ndani wakifanya ufuska wao.
Mshale wa saa ukazidi ukapiga hatua nyingine, Tinonko akasikia lile vuguvugu la hewa isiyotulia ikiwa kimya kabisa, mara akasikia kitu kikimfinya mkononi kama alivyoambiwa, akafungua macho.
Je, Tinonko amefika nyumbani kwake? na kama amefika atafanya nini?


ITAENDELEA IJUMAA

Post a Comment
Powered by Blogger.