NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI NA SITA(16)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu. • Kapteni Tinonko akiwa na upweke wa kuachana na wenzake, aliendelea kutafakari nini cha kufanya baada ya kutengana nao kwa namna hiyo ya ajabu.
  “Aka-Baka anadhani naweza kufanya kazi hii peke yangu?” alisema Kapteni Tinonko akimuuliza yule mtafsiri wa Aka-Baka.
  “Ndugu yangu wewe ndiye uliyetoka Mashariki na umeletwa kwetu ukiwa na mikono kumi hatujakosea,” alijibu yule Mbirikimo hilo likamshtua tena Kapteni Tinonko.
  “mwambie Aka-Baka nini ninachotakiwa kufanya? Nahitaji kurudi nyumbani.” Alisema Tinonko kwa sauti ya kuishiwa uvumilivu.
  Yule mbirikimo haraka akamnong’oneza Aka-Baka naye akamjibu jambo la kumwambia Tinonko. “Anasema tutaenda leo usiku lakini kuna dawa maalumu anataka kukuonesha kabla ya kwenda huko.”
  Kwa maneno hayo ndipo Aka-Baka sambamba na Twa na Tinonko peke yao wakaelekea kwenye maporomoko fulani ya maji. Aka-Baka akayapiga yale maji kwa fimbo yake likajiumba wimbi dogo na hatimaye likakua na kupotelea katikati.
  Katikati akaonekana mfano wa samaki mdogo wa mwekundu akiwa anaogelea kuja alipokuwa Tinonko, Aka-Baka akasema mchukue ule. Kwa maneno hayo Tinonko hakuuliza kwa kuwa ameshajionea maajabu ya kutosha kumfanya mtu awe chizi, hivyo akatosa mkono kwenye maji na kumshika yule samaki aliyeonekana kama vile hataki kukimbia.
  Mkono wake ulipomtoa nje ya maji alionekana mkavu kama vile amekaushwa kwa moto tayari kwa kuliwa.

 • Akammega na kula kipande baada ya kingine hadi akaisha na kubakiwa na mifupa pekee.
  Baada ya hayo Aka- Baka akasema, mwenye jicho la umauti hatakuona, sasa unaweza kuingia katika ile kambi na kumleta mtoto wetu kwetu bila mtu kukuzuia. 
  Hiyo mifupa ya samaki unatakiwa kumchoma nayo, Ntaganda shingoni mwake, hapo yeye na wafu wenzake watarudi kuzimu walipotoka ukimaliza kufanya hayo utarudi nyumbani kwako kwa mwendo wa kufumba na kufumbua.
  Jackline akiwa hana lile wala hili alijipara vya kutosha na kuandaa chakula kizuri akipendacho Peter, kisha akamtaka Suzy amsaidie kwa mambo kadhaa hasa kufagia na kusafisha vizuri baadhi ya sehemu.
  Wakiwa wamemaliza maandalizi yao ghafla walisikia mlango ukigongwa, wote wakajua ni Peter hivyo Jackline aliyejaa kisebusebu akainuka haraka na kwenda kuufungua mlango kwa shauku huku amejiandaa kwa tabasamu pana la karibu mpenzi.
  Lakini kinyume na matarajio yake alishangaa kuona mlinzi wake wa getini, “mama leo ndiyo tarehe ya simba kupelekwa kwa daktari wake kwa ajili ya chanjo ya kichaa, Husseni amekuja kumchukua,” “Sawa mwambie amchukue,” alisema Jackline na Suzy akadandia kwa juu, “Tena mwambie huyo daktari, huyu mbwa ni kichaa kabisa tena akae naye hukohuko hata hatumtaki!”
  “Anakutania amrudishe,” alisema Jackline na kumvaa rafiki yake; “wewe Suzy kwani una nini? Huyu mbwa ndiyo kumbukumbu ya mume wangu halafu majambazi wakija hapa we unafikiri nani atatulinda?”alisema Jackline bila kujua majambazi ndiyo hao alionao hapo ndani.
 • Wakati wanaendelea walisikia kelele za Simba kidogo kisha baadaye kukawa kimya, ikaonekana kama vile ameshapelekwa huko hospitali na Hussein.
  Baada ya dakika chache mlango uligongwa tena, walipoufungua safari hii ndiyo Peter alikuwa anaingia, Jackline akamrukia na kumkumbatia kwa furaha kisha akamkaribisha kwa bashasha kama vile ambavyo angepaswa kumfanyia mumewe Tinonko.
  Mahawara wawili wasiojijua wakala wakasaza, wakanywa na sasa ikafikia zamu ya kwenda kufanya uhaini chumbani kwa mume wake tena juu ya kitanda cha Tinonko. Wakati huo wote jicho kali la Suzy lilikuwa likimtoka akifuatilia kila hatua ya Jackline na mpenzi wake Peter, tena mara nyingine nusura aharibu lakini Peter akamkonyeza, akapoa.
  Giza lilianza kutanda kuashiria usiku wenye kiza kinene, Tinonko akasimama na kuingia kwenye kambi ya wale waasi kama alivyoambiwa na wenyeji wake, moyoni mwake akitaka kufanya kila linalowezekana amalize kazi hiyo mapema na kurudi nyumbani Tanzania kama alivyoahidiwa.
  Akavuka na kutembea taratibu na kupenya katikati ya kundi la wale wanajeshi wakilinda doria lakini cha kushangaza kama vile alivyosema Aka-Baka, safari hii hakuna mtu aliyeweza kumuona akiwa anapita mbele yao.
  Akaingia na kuvuka kila sehemu ndani ya kambi hiyo yenye harufu kali ya mizoga ya watu walio hai, hatimaye aliweza kumuona mtoto mdogo wa kiume akiwa katika moja ya mahema pembeni yake akiwa ameketi Temineta Ntaganda, akiwa ameganda bila kufumba macho.
 • Bila kusubiri Tinonko akachukua mfupa mmoja wapo wa yule samaki na kuushindilia ndani ya shingo ya Ntaganda palepale akadondoka chini kama mzoga, kisha akamchukua yule mtoto ambaye alionekana kiumri chini ya miaka minne akaondoka naye moja kwa moja kutoka nje ya ile kambi.
  Nje mizoga ya wale wanajeshi wa Temineta ilikuwa imezagaa kila eneo. Hilo lilimpa furaha sana, tayari alikuwa akiona anarudi nyumbani tena na kukutana na familia yake.
  Huko kijijini kwa mbirikimo kulikuwa na sherehe kubwa ya kupokelewa kwa wapendwa wao, na kwa kuwa Tinonko alifanikisha kila kitu basi naye akawa kiini cha furaha hiyo.
  Lakini sura ya Aka Baka haikuwa na hisia zozote za furaha kila alipomuangalia Tinonko, baadaye akamuita pembeni akiwa na yule mtafsiri wake.
  “Kapteni, kuna jambo Aka-Baka anataka kukuonesha, pengine litakufanya usitamani hata kurudi nyumbani kwako kwa sasa,”
  “Unasemaje? Ninataka kurudi haraka nimefanya mliyoniagiza naomba na nyinyi mnitimize ahadi yenu kwangu!” alifoka Tinonko.
  “Aka-Baka anasema jambo litakalokuzuia ni kutoka ndani ya familia yako mwenyewe. Kuna watu hawataki uwe hai na ndiyo wamekufanya hadi uwe hapa. Pindi ukionesha sura yako sasa wakati hauwajui na kitu gani wanachokitafuta kwako, nadhani utakuwa kama vile unaingia kwenye mdomo wa mamba.” “Sielewi unachosema,” alisema Tinonko. Aka-Baka akachukua kitambaa cheupe na kutemea mate, kikawa kama tivii. Ndani yake akaonekana Jackline akifanya mapenzi na Peter tena chumbani kwake,” Aka-Baka akafanya kama vile anapangusa kile kitambaa, akatokea mama yake mzazi akiwa hospitali amelala hoi. Akapangusa tena hapo akaonekana mtu aliyevaa nguo za jeshi akiwa na picha ya Tinonko, kisha kile kitambaa bila kuonesha mtu huyo alikuwa ni nani kikawa kama vile kimekata mawasiliano.
ITAENDELEA JUMATANO
Post a Comment
Powered by Blogger.