NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI NA TATU(13)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Siku hiyo Jackline alirudi nyumbani kwake usiku ikiwa siyo kawaida yake hata kidogo, pengine kungekuwa na mtu wa kumhofia angeweza kuwa na wasiwasi, lakini hakukuwa na Tinonko na mama mkwe wake yu hoi taabani hivyo hakuwa na wasiwasi wowote.
Akaingia ndani huku mlinzi akifungua na kufunga geti kwa adabu. Mwanamke wa watu akaingia hadi sebuleni. Macho yake yakakutana na Suzy aliyeanza kusinzia pale kwenye kochi.
“Enhe vipi shoga mambo yamekuwa mambo!” alisanifu Suzy.
“Ndiyo kwa raha zangu,” alijibu Jackline huku akiachia tabasamu pana lililoashiria raha alizozipata muda mfupi uliopita.
“Weeeh! basi mmekumbushiana hadi basi, hahaa si muoane sasa au?” alisema Suzy macho yake yakiwa makavu baada ya kugundua rafiki yake alikuwa ananukia kilevi.
“Kwani nina ugomvi na mtu, niachege kwa raha zangu,” alisema Jackline lakini akakatishwa na kishindo chumbani kwa mama mkwe wake akasimama na kuelekea haraka nyuma yake Suzy akimfuata.
Mama yake Tino alikuwa amedondoka chini kutokea kitandani, sauti yake ilikuwa imekauka mno kiasi cha kutosikiwa ikitoka, alionekana fika kuwa amezidiwa.
Pombe zote zilimtoka Jackline akakimbilia simu yake na kupiga hospitali ya Lugalo ambayo familia yake ilikuwa ikitibiwa bure kwa kibali cha jeshi.
Ndani ya dakika kumi, Ambulance ilikuwa imefika na kumchukua kisha safari ikaelekea hospitali. Baada ya vipimo vya awali mama Tino aligundulika kuzidiwa kwa kukosa chakula na maji kwa muda mrefu jambo linalofanya dawa kali anazozitumia kumnyong’onyesha.


“Lakini dokta mbona chakula ninampa kila siku,” alilalama Jackline.
“Vipimo havidanganyi binti, una uhakika?” aliuliza daktari huyo wa jeshi ambaye amekuwa akimtibia mama huyo tangu matatizo yake yalivyoanza.
Jackline akafunga mdomo wake baada ya kugundua kuwa siku hiyo alimuacha mgonjwa na Suzy pekee hivyo huenda Suzy hakuwa amempa chakula.
Akainamisha kichwa kwa aibu na kukubali ushauri wa daktari kuwa anatakiwa kumuangalia sana mgonjwa huyo, lakini hata hivyo alitakiwa amuache hospitali hapo hadi hali yake itakapotengemaa kwa kuwa alikuwa mahututi.
Hasira zake zilimuishia rafiki yake, Suzy ambaye kwa aibu aliishia kumuomba msamaha rafiki yake. Ndani ya dakika chake Jackline alimkubalia rafiki yake huyo na kujiendea zake kulala kwa kuwa ilikuwa ni usiku mno.
Wakati huo Suzy akaingia chumbani kwake na kumpigia simu Peter wakipanga mambo yao.
“Huyu mwanamke ananipanda kichwani bwana, natamani tumalize haya mambo tuondoke zetu,” alisema Suzy kwa hasira, kumbe wakati ule alimuomba msamaha rafiki yake kinafiki tu.
Wakati huo Simba aliyekuwa akirandaranda uani alizunguka na kusimama usawa wa dirisha la Suzy na kuanza kubweka kwa sauti. Suzy ambaye kwa wakati huo alishajua haendani damu na mbwa huyo hivyo akapuuza na kuendelea na maongezi yake.
“Sikia Suzy, huyo nimeshamuweka mkononi, bado kidogo tu kila kitu kikamilike, yaani kwa mapenzi niliyompa leo mwenyewe anataka kuchomoa hiyo mimba.” Alisema Peter.

“Wee! Kweli! Mh ..mbona naanza kujisikia wivu, mapenzi gani uliyompa tena. Usije tu ukampenda kiukweli ukaniacha peke yangu,” “Wewe ndiyo kila kitu kwangu, cha msingi endelea hivyohivyo, huyo anatakiwa ajue kuwa mimi na wewe ni mtu na dada yake kama kawaida, usiharibu wala usilete wivu wako wa kijinga tukaharibu hii kazi,” alisema Peter.
“Sawa mpenzi wangu, kwa hiyo mmepanga lini mnaenda kuitoa hiyo mimba?”
“Aliniambia hata leo lakini nimemwambia tufanye wiki ijayo, amekubali,”
“Haya, lakini kikwazo hapa naona huyo mama yake maana anaumwa lakini kufa hafi na ndiyo anayemfanya saa nyingine asitesite kufanya mambo, kama vipi umalizage bwana,” aliongea Suzy akimwambia Peter ambaye muda wote tulifahamu kuwa mtu na dada yake, kumbe wapenzi hatari. Maskini Jackline wa watu hata hajui chochote.
“Hilo usijali nina marafiki zangu madaktari pale Lugalo ngoja nitamaliza. Mbona hapo ulipo kuna makelele hivyo?”
“Aagh! Hapa kuna hili limbwa kama limetumwa yaani likinisikia tu linanipigia kelele kweli.” alisema Suzy kisha wakaagana na mpenzi wake akazima taa na kulala akiota ndoto za utajiri.
***
Kapteni Tinonko akiwa amefungwa na wenzake pale kwenye vizingiti, kila mmoja akisali sala lake kujiandaa na huko waendako, mara wakasikia hatua ndani ya chaka zito lililokuwa nyuma yao.
Kutokana na usiku kuwa na giza sana, walihisi moja kwa moja huenda akawa ni mnyama mkali. Kama wanajeshi kamili waliombea wafe mikononi mwa huyo mnyama wa mwituni kuliko kwenye mikono ya Ntaganda.

Hatua zilizidi kusogea na kujipambanua kuwa ni za wanyama wengi, sasa kadri vishindo vilivyozidi kusogea, nao wakafumba macho wakikikaribisha kifo.
Kwa mshangao walishangaa kuwaona wale mbirikimo wakiongozwa na Aka –Baka na Twa tena wakiwa na majani ya ajabu mikononi mwao.
Wakapita kwa kila mmoja wao na kuzipiga kwa ujani zile nyororo, cha kustaajabisha zikafunguka kama kamba zilizooza kisha wote wakatoroka na kutokomea maporini mbali na upeo wa ile kambi.
Wakiwa huko, Aka –Baka akachukua dawa fulani na kuwanusisha wale makomando wanne waliojeruhiwa palepale wakarudiwa na nguvu na yale madonda yao yakapakwa madawa ya ajabu.
Wakiwa wametumbua macho bila kusema chochote, wakapewa chakula ambacho ni nyama ya swala wa porini na kula kwa kiasi chao, kisha usingizi mzito uliojaa ndoto za kutisha juu ya maajabu waliyojionea Congo zikiwaandama.
Jua la kwanza kuchomoza liliwashtua na kwa mara ya kwanza kila mtu akajikagua na kujiona ni mzima na imara hata yale majeraha yalionekana kupotea yote, hapo wakawa na nguvu ya kuwauliza wenyeji wao wa kimbirikimo juu ya wale waliyoyaona.
Wakacheka kisha Aka-Baka pekee akajitokeza na kuwafafanulia, wakabaki vinywa wazi kwa maajabu waliyoyasikia.


ITAENDELEA JUMAPILI
Post a Comment
Powered by Blogger.