NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI NA MOJA(11)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Moja kwa moja Kapteni Tinonko na makomando wake wanne waliobakia waliingizwa katika vibanda vilivyofungwa sawasawa kwa miti migumu ya msonobali na kushindiwa ipasavyo ardhini. Urefu wa kibanda hicho uliweza kuwafanya wasisimame zaidi ya kukaa au kulala kwa kuwa vilikuwa vifupi mno.
Tinonko alijitahidi kuwahudumia makomando wenzake ambao wengi wawili kati yao walikuwa wamejeruhiwa sana, kwenye muda huu hakika hakukuwa na muda wa kuhuzunika wala kuombeleza kwa wale wenzao waliokuwa wamepoteza maisha mbele ya silaha ya jeshi la waasi wa Ntaganda ambao walionekana hawadhuriki.
Swali la msingi lililojirudia kichwani mwake ni kwamba inawezekanaje mtu kama Ntaganda ‘Temineta’ waliyekuwa na uhakika walimmaliza akaishi tena akiwa na nguvu zake kama vile hakukuwa na jambo lililomtokea?
Hilo likamfanya ahisi huenda yule alikuwa ndugu yake na si mwenyewe halisi. Hapo akakumbuka kuwa mara kadhaa kuwa alishawahi kusoma kwenye baadhi ya vitabu vya kijasusi kuwa viongozi wengi hasa wa Urusi ya Zamani ‘USSR’ walikuwa wakitumia watu wengine wanaofanana nao kwenda kwenye mikutano ya wazi wakiwa na mashaka, hiyo ni kuwasaidia wasiuawe wao pindi njama za mauaji zitakazofanywa na maadui zao.
Hiyo inaweza kufanyika hata kwa viongozi wengi wa kiafrika siku hizi, hivyo Kapteni Tinonko alihisi huenda uwepo wa Ntaganda akiwa katika uzima wake ilikuwa pengine ni njia hiyo.
Akiwa katika mawazo haya alishuhudia giza likizidi kutanda ndani ya msitu huo waliopo, akawakumbuka wale wapiganaji wa Kimbirikimo lakini hakuwaona siyo kwenye upande wa waliohai wala kwa wafu, akahisi kuna walakini.
Akafumba macho akimkumbuka mkewe Jackline na mama yake mzazi akaomba Mungu awalinde kisha shujaa wa vita akapitiwa na usingizi mzito.


Siku ya pili asubuhi, Jackline alianza kwa kufanya kazi zake za nyumbani akisaidiwa na Suzy, akiwa katika haraka ya kukutana na Peter alihakikisha anamuachia Suzy bajeti nzima ya chakula cha siku na kukumbusha kumpikia mama mkwe wake, ndizi laini za Bukoba kwa kuwa tangu aanze kuumwa hakuweza kutafuna.
Kwa fedha nyingi alizoachiwa kwenye akaunti na mumewe, Jackline aliweza kuchukua kiasi kidogo sana kukodi teksi hadi baa ya Mapozeo ambayo waliahidiana kukutana na Peter saa sita ya mchana siku hiyo.
Japo kuwa ni mke wa mtu lakini alishindwa kujizuia kuhakikisha Peter anamuona katika ubora wake, japo kuwa ukweli ni kwamba alikuwa amenenepa sana kutokana na mimba yake changa kiasi kwamba ile shepu yake ya awali ilipotea.
Alifika na kushuka akaitazama saa yake kwenye simu na kuona ilikuwa ni saa sita na dakika kumi na nane, akaona ni muda muafaka kwa kusababu hakutaka kiraruraru chake kimfanye awahi kuliko hawara mwenzake.
Akaingia upande wa baa na kupitiliza moja kwa moja hadi upande mwingine ambao ulikuwa umejificha zaidi, akiwa anaangaza kila upande, mara akasikia mtu anamuita, akageuka macho yake yakakutana na Peter, bado ni hendsam kama kawaida tena alionekana kuvutia zaidi kutokana na mavazi yake hasa kifulana chake cha mikono mifupi kilichoacha wazi mikono yake yenye misuli mingi.
Akiwa katika msisimko wa penzi, Jackline alitembea kwa pozi na kwenda moja kwa moja hadi alipokaa Peter na kukaa huku akimtazama bila kuongea neno lolote, Peter aliyeonekana muda wote anatabasamu akamshika begani Jackline, akamuita kwa jina la enzi za mapenzi yao, “Mei, mambo?”

“He! Wewe unalikumbuka tu jina hilo, Jamani!” alijibaraguza Jackline japo kuwa kwa kuitwa hivyo alijikuta akikumbushwa mbali sana.
“Kwa nini nisikumbuke? sijasahau hata kitu kimoja kuhusu wewe?” alisema Peter huku tabasamu lake lililoficha jambo likiwa wazi muda wote.
“Mh, muongo! kama kweli niambie siku yangu ya kuzaliwa ni lini?” “ni tarehe 6 mwezi wa nane, nimalizie na mwaka?”
“mh umetisha kha!”
“enhe tuache yote hebu niambie ulichoniitia,” alizungumza Jackline huku kile kitendo cha Peter kukumbuka birthday yake kikizidi kumchanganya.
.........
Huku nyuma mara baada ya Jackline kuondoka, sauti ya kigonjwa ya mama yake Tinonko ilisikika ikiomba maji. Suzy aliyekuwa bize na simu yake alitulia kimya, lakini kadri mama Tino alivyokuwa akirudia ombi lile Suzy alionekana kukerwa na hali hiyo akainuka akiwa na hasira na kumkoromea mgonjwa wa watu apendavyo.
Sauti hiyo kali ikapenya ndani ya masikio ya Simba akabweka kwa sauti kana kwamba anataka kuvunja banda, cha ajabu mara baada ya Suzy kunyamaza sauti ile ya mbwa ilitulia.
“huyu mbwa ana nini na mimi, mbona hata nikitokaga nje huwa ananipigia sana makelele?” alijiuliza kimoyomoyo na kurudi alipoketi lakini hakupeleka maji hata kidogo.
…..
Kapteni Tinonko akiwa na wenzake alishtushwa asubuhi hiyo na askari wa Ntaganda waliofungua kibanda na kumtoa Tinonko.
Akachukuliwa juujuu hadi kwa Temineta Ntaganda.
“Wewe nakujua!” alisema Ntaganda kwa Kiswahili cha Kikongo.
Neno hilo likamfanya Kapteni Tinonko atulie kimya akijiuliza huyu mtu alishawahi kuniona wapi?
“Wewe uliniua, ukanipiga risasi hapa,” alizungumza Ntaganda na kuvua kombati yake akaonesha mashimo ya risasi tumboni na jingine kifuani, cha ajabu mashimo yale yalionekana makubwa na yalikuwa yakitoa harufu kali na wadudu. “Nadhani ulishajuaga vile kwanini naitwa Temineta Ntaganda,” alisema na kucheka kicheko cha kishetani. Hilo likamfanya Kapteni Tinonko aogope na kujiuliza, anaota au?

ITAENDELEA IJUMAA
Post a Comment
Powered by Blogger.