NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KUMI(10)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kina Kapteni Tinonko waliambiwa na wenyeji kuwa mtoto huyo wanayetakiwa kumuokoa ana uwezo wa ajabu wa kutibu na kugundua mambo ya kiasili yaliyofichwa ndani ya msitu wa Congo. Hivyo waasi walivamia kijiji chao na kumteka mtoto huyo kwa kuwa walimtaka awaoneshe machimbo ya dhahabu na kuwasaidia kushinda vita na mambo mengine ya kimizimu.
Twa alisema kuwa mtoto huyo alikuwa muhimu kuokolewa kutoka mikononi mwa waasi hao kwa kuwa kama atatumia nguvu zake itakuwa hatari kwa Congo nzima kwa kuwa waasi hao watakuwa ni jeshi lisilopigika na kuweza kufanya kila kitu wanachokitaka.
Kitu kikubwa walichotakiwa kufahamu ni kwamba, mtoto huyo ambaye huzaliwa kwenye jamii ya kimbirikimo kila baada ya miaka mia tatu, yupo katika mikono ya watu wabaya na kwa kuwa hajui baya na jema anaweza kufanya chochote kwa kuwa hajafundishwa na desturi na Aka Baka.
Hatua moja moja makomando wa Kapteni Tinonko walisonga, kwenye kiini cha ile kambi. Kuna sehemu walilazimika kujificha kutokana na mwanga mkubwa wa kurunzi la mwanajeshi mlinzi aliyepitapita huko na huku kuzungukia mipaka.
Walitambaa bila kelele hatua kadhaa nyuma wakiwa na wale wapiganaji wa kimbirikimo waliokuwa na mishale yao ya sumu kali.
Wakiwa wanajiandaa kwa mashambulizi ghafla ukelele mkubwa ulisikika kutoka nyuma yao, kisha risasi zikaanza kupenya kwenye hewa , wakawa ndani ya mashambulizi makubwa.
Ilionekana kama risasi zao zilikuwa zikidunda juu ya miili ya kundi lile la wanajeshi waasi lakini zao ziliwajeruhi na kuwadondosha chini kama mabua. Kutahamaki walikuwa wamezungukwa kila kona huku makomando wake karibia wanne wakiwa wamejeruhiwa vibaya na sita kati yao wakiwa wamekufa papo hapo akiwemo yule rubani.


Kapteni Tinonko akiwa ameweka mikono kichwani kama ishara ya kukubali kushindwa ‘Sarenda’ alichukuliwa kama mzoga na wale makomando wake wanne akiwemo Niko na hatimaye kuswekwa kwenye chumba kidogo hali wakiwa wamefungwa kamba ngumu.
“Waacheni hapo mupaka mukulu aje!” alisema moja wa waasi wale aliyeonekana kama kiongozi wao.
Ndani ya dakika chache gari aina ya Jeep ya kivita iliingia ikiwa na wanajeshi wachache ndani yake, moja kati yao alikuwa ni mtu ambaye Kapteni Tinonko alidhani kuwa anamfahamu vizuri.
Japo kuwa ilikuwa usiku lakini upara wake mng’avu na umbile lake, alionekana ndiye yeye kabisa, mwanga wa mwezi ukammulika upande mmoja wakati akiongea na yule muasi mtwana aliyekuwa akitoa amri muda mchache uliopita.
Uthibitisho wa wazo la Kapteni Tinonko ulipatikana baada ya yeye kuja hadi alipo na kumtazama kwa makini, “Ndiye yeye Temineta Ntaganda!”
“Ina maana tuliyemuua kule Kivu alikuwa ni nani? mbona alifanana kila kitu na huyu bedui?” alijiuliza kimoyomoyo Kapteni Tinonko wakati huo Ntaganda akifungua kinywa chake kichafu na kucheka kama mwenda wazimu; “Ha Haaa Haaa!”
…..
“Peter, Jackline anaonekana kusitasita sana kwenye hili jambo, mimi naona tumalize kazi tuondoke zetu atatuangusha bure huyu!” ilikuwa ni sauti ya Suzy akizungumza na kaka yake Peter kupitia simu yake.
“kwa nini inakuwa hivyo? Mwanzoni nadhani uliniambia vizuri tu kuwa hatuna tatizo lolote inakuwaje hivyo sasa?” ilikuwa ni sauti nzito ya Peter.
“Amejua kuwa yumo kwenye mirathi ya mume wake ikiwa atamzalia mtoto, sasa tunafanyaje?” “Anha, hilo tatizo niachie mimi, cha msingi wewe mwambie nataka kuonana naye kesho kwenye Baa ya Mapozeo, akikubali niambie,” alisema Peter na kukata simu.
Suzy harakaharaka akainuka na kurudi ndani ya nyumba kwa kuwa simu ile aliipokelea nje ya geti kwa kuwa hakutaka mpango wao mchafu aujue Jackline.

“Jackline, kisia nini!” alisema Suzy akionekana kuwa na furaha wakati saa chache zilizopita alikuwa ameondoka akiwa amenuna kweli.
“sijui, niambie,” aliongea kiuchovu Jackline akiwa amejilaza kwenye kochi akiangalia taarifa ya habari ya usiku.
“Peter amenipigia amesema ni kusalimie,” alifunguka Suzy, kwa neno hilo likamfanya Jackline akae vizuri kitini na kumsikiliza vizuri Suzy.
“enhe..”
“Ndiyo hivyo anakusalimia na amesema anatamani akuone japo mara moja kesho pale Mapozeo.”
“umeongea naye kwenye simu au?” “Ndiyo, tena anaonekana anakukumbuka kweli yaani, si unajua mpaka sasa hana mtu yoyote tangu ummwage,” alikandamiza Suzy na kumfanya Jackline aheme juujuu huku akikumbuka mapenzi yao motomoto enzi hizo.
Hakujibu lakini moyoni alikuwa kama amechochewa moto, hakulala kwa amani alitamani na yeye amuone Peter hiyo kesho kwa kuwa hakuonana naye kwa siku nyingi sana, kifupi alikuwa amemmisi sana.
“Wuuh wuuh!” zilikuwa ni kelele za Simba akibweka, hapo ndiyo akakumbuka kuwa ni muda wa kumfungulia kutoka bandani kwake maana kila ifikapo saa 5 usiku hufunguliwa na kurandaranda hapo uwani akimsaidia mlinzi.
“kwa hiyo utaenda?” aliuliza Suzy kinafiki.
“ndiyo kwa nini nisiende au kuna ubaya kusikiliza wito?” alijibu Jackline hali akijua si wito tu maana chochote kinaweza kutokea.
Mara baada ya kuhakikisha fitina zake zimefika, Suzy akasimama zake na simu yake mkononi na taratibu akatoka zake nje ili kumpa taarifa kaka yake kuwa mtoto wa watu yu hoi taabani kwa ajili yake.
Akiwa amefungua mlango na kupiga hatua chache alijikuta akipiga kelele baada ya kuvamiwa na Simba ambaye almanusura amlarue vibaya. Badala yake akaishia kuchana vibaya kigauni chake, salama yake ni kurudi ndani na kufunga mlango haraka huku kilanga chake kikimuisha.

ITAENDELEA ALHAMISI
Post a Comment
Powered by Blogger.