NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA PILI(2)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Ilikuwa mwezi, ikawa wiki na maandalizi yalikuwa yamekamilika kwa ajili ya harusi ya kipekee kati ya Bwana Tinonko Marato na Bibi Jackline Kimaro, michango yote ya harusi tayari ilikuwa imeshaifikia kamati ya maandalizi na hatua za mwisho tu ndiyo zilikuwa zikisubiriwa.

Kutokana na suala la ndoa ya kapteni Tinonko kufika kazini kwake, jeshini, kapteni alipewa barua ya likizo ya wiki mbili nzima ili kufanikisha vyema suala lake la ndoa. Siku chache baadaye wageni na ndugu kibao walikuwa wakimiminika nyumbani kwa Kapteni Tinonko, wakati huo Jackline alikuwa nyumbani kwa wazazi wake kwa sababu kimila ilikuwa lazima watengane kwanza miezi michache kabla na kuungana tena baada tu ya kufunga ndoa.
“Mwanangu huyu mbwa wako siku hizi amekuwa na makelele kweli, hadi anawatisha wageni, hebu kamnyamazishe kwanza,” alisema mama yake Kapteni Tino. 
Mwenyewe akaenda pale bandani na kumtazama mbwa wake kisha akazungumza naye kama vile anaongea na binadamu mwenzake; “Simba nini tatizo? Mbona una makelele sana,”
Yule mbwa akamtazama bosi wake na kutoa sauti ya mbwa mpole, hapo Kapteni Tino akacheka na kusema; “usipige makelele hawa wageni wanakuja kwa ajili ya harusi yangu na Jackline,” alisema Kapteni Tino na yule mbwa akabweka kwa sauti ya chini kidogo.
Wakawa kama vile wanaelewana katika maongezi yao. Hiyo haikumshangaza mama yake Tino kwa kuwa mara nyingi Tino alikuwa na urafiki mkubwa na yule mbwa kiasi kwamba huweza kuzungumza naye na wakaelewana kama vile wanadamu wawili.

Harusi sasa ilikuwa inatarajiwa kufungwa kesho yake katika kanisa la St. Peters Oysterbay. Asubuhi hiyo wanaharusi walikutanishwa kwa ajili ya mazoezi na kupewa taratibu zote zitakazofanyika kesho yake.
Kapteni Tino na Jackline wakiwa na moja wa wanandoa watarajiwa walifika na kushiriki utaratibu huo chini ya usimamizi wa Bwana Oswin Kizito na mkewe Bi, Mary Magesa.
Walimaliza utaratibu zote na kila mmoja kurudi nyumbani tayari kwa siku ya tukio kubwa siku iliyofuatia, Kapteni Tino alionekana mwenye furaha kubwa kwa sababu siyo tu alikuwa anatimiza moja ya ndoto za maisha yake ya kumuoa msichana anayempenda, bali pia alikuwa akifanya tendo hilo akiwa na baraka tele kutoka kwa mama yake mzazi.
Kwa upande wa Jackline naye alikuwa hivyohivyo, furaha yake ilitokana na kufikia malengo yake kama mwanamke, akamshukuru Mungu kwa hilo kwa kuwa marafiki zake wengi walikuwa hawajabahatika kuolewa japo wanatamani sana.
Akatumia muda huo kuwaza jinsi alivyoweza kuacha mambo yake kando ikiwemo kuachana na wanaume wake wote akiwemo Peter ingawa alikuwa akimpenda kwa dhati, lakini mwanaume huyu hakuwa siriasi kwenye suala la ndoa na alionekana bado hajamaliza mambo ya ujana.

Kama kawaida, taratibu zilianzia asubuhi saluni na safari ikahamia kanisani ambapo saa 8 mchana ilikuwa ndio muda wenyewe.
Padri alianza kwa kusoma misa ndefu na hatimaye ikafikia wakati wa wanaharusi kufunga pingu zao za maisha. Kwa kuwa kulikuwa na harusi tatu siku hiyo ikiwemo harusi ya Kapteni Tino. Kidogo ilichukua muda lakini sasa wakiwa katikati ya misa ya harusi hiyo ghafla alitoka mtumishi mmoja kutoka nyuma kabisa ya kanisa na kuwahi haraka mbele kwa padri kisha akamnong’oneza jambo.
Akaonekana kama vile amepigwa na butwaa, akaanza kupeleka matukio harakaharaka na ndani ya dakika mbili, harusi ya Kapteni Tinonko ilifanywa ya kwanza na kufungwa kisha wakarejea kwenye kiti, hakuna mtu aliyejua sababu ya padri kufanya vile lakini baadaye kapteni aligundua baada ya kuitwa haraka nje ya kanisa.
Alitakiwa kuaga familia yake haraka na kujiandaa ndani ya masaa mawili kwa ajili ya kusafiri kuelekea kwenye oparesheni nchini Kongo DR, akaambia kuwa amechaguliwa kuwa mmoja wa waongoza kikosi cha wanajeshi kutoka Tanzania wanaotakiwa kulinda amani nchini humo wakiwa chini ya ndani ya vikosi vya umoja wa kimataifa UN.
Ndani ya masaa manne yaliyofuata tayari alikuwa kwenye dege la jeshi akiiacha ardhi ya Tanzania.ITAENDELEA JUMATANO

Post a Comment
Powered by Blogger.