NAJUTA KUMSALITI MUME WANGU SEHEMU YA KWANZA (1)

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Tino aliamka akiwa na furaha kubwa ya ndoto yake ya muda mrefu kutimia. Ndoto hiyo si nyingine bali ni kupanda cheo kipya jeshini. Hakuwa akidhani katika umri mdogo kama wake angeweza kufikia cheo cha Ukapteni.
Hiyo haikuwa ni kazi nyepesi, ni baada ya kujibidiisha katika mafunzo mbalimbali ya kozi za kijeshi alizofaulu vizuri akiwa nchini Urusi, Uingereza na China.
Hiyo ilimfanya hata Jenerali Martin kuutambua uwezo wake na kumpandisha vyeo haraka akinzia ngazi ya ukoplo.
Akavaa magwanda yake vizuri aliyoandaliwa na mpenzi wake, Jackline na kufungua kinywa kisha akatoka himahima na kwenda kuwasha gari yake aina ya Toyota Noah na kuipasha moto injini wakati akimsubiri mama yake mzazi na mchumba wake Jackline waingie.
Kama kawaida waliingia taratibu lakini ilikuwa ngumu kidogo simba kukubali kubaki peke yake pale nyumbani.
“simba kaa chini!” ilikuwa ni sauti kali ya Tino ikimuamrisha mbwa wake mtiifu simba kubaki pale nyumbani, naye akakaa kimya uso wake ukionesha huzuni mkubwa.
Ndani ya dakika mbili tayari walikuwa safarini kuelekea makao makuu ya Jeshi Upanga.
Walifika na kupaki gari kisha wakashuka huku  Tino akiwaelekeza wakakae sehemu walizoandaliwa wageni watakaohudhuria sherehe hizo kwa siku hiyo.
Tinonko naye aliambatana na wenzake waliokuwa ndani ya magwanda yao, wakajipanga na kukaa siti za peke yao wakisuburi shughuli ianze.
Wakati huo wote bendi ya jeshi ya matarumbeta maarufu kama Brass Band ilikuwa ikitumbuiza nyimbo kadhaa za kizalendo.
Ilisemekana kuwa rais mwenyewe atakuwepo hapo siku hiyo, hivyo kila mtu alikuwa bize kuhakikisha hakiharibiki kitu.
 Muda wote huo wageni waliokuja kushuhudia ndugu zao wakipanda vyeo walikuwa wakishangaa jinsi wanajeshi walivyokuwa wakifanya mambo yao kwa ukakamavu kweli.
 Na hii ilimshangaza hata Jackline mwenyewe ambaye aliona kwa mara ya kwanza, mtu mzima sana akimnyenyekea kijana mdogo kiumri. Hapo ndiyo mama yake Tino ambaye kidogo alikuwa na uelewa wa masuala ya kijeshi kupitia mwanaye, akamfafanulia Jackline kuwa heshima hiyo ilitokana na alama ya vyeo vyao walivyovibeba mabegani mwao.
Ndani ya muda mchache walianza kukaribishwa kwenye shamrashamra na baadaye rais wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, alifika na kupita juu ya zuria jekundu kisha akaenda kuketi kwenye jukwaa.
Shughuli ikapamba moto kwa kupitia vipengele kadhaa vinavyoboa ikiwemo kusoma risala ndefu yenye maneno kibao ya misamiati.
Jackline na mama yake Tino wakajikuta wakipokezana kupiga miayo hadi mwishowe wakasinzia.
Walishtushwa na vigeregere na vifijo kutoka kwa watu waliowazunguka walipoamka waligundua ilikuwa ni zamu ya rais kutoa vyeo kwa wanajeshi hao na tayari alikuwa ameanza.
Walisubiri majina mengi yakipita na hatimaye ilifika zamu ya mwanaye, Tino akasikia anatajwa; Tinonko Marato. Mwenyewe akasimama kwa ukakamavu kutoka pale kwenye kiti chake, akatembea hatua za kijeshi kufuata lile zuria jekundu kisha akapiga kwata na kusogea mbele ya rais aliyekuwa amesimama katikati ya viongozi wengine wa kijeshi.
Akawekewa nyota mabegani na kurudi kwa mwendo uleule hadi kwenye kiti chake. Hii ilikuwa ni furaha kubwa kwa mama Tino na Jackline; walikula na kunywa kisha sherehe ikahamia nyumbani kwao.
“Mwanangu baba yako angekuwepo angefurahi sana hata mimi nimefurahi sana, lakini nataka unifurahishe zaidi, muoe huyu binti ili mniletee wajukuu, sitaki muishi hivi tu,” alizungumza mama yake Tino akimwambia mwanaye wakati huo Jackline akiwa bize kuandaa Juisi ya mapasheni huko jikoni.
 “Mama hata mimi mwenyewe nimelifikiria hilo, hamna tatizo, tuanze na kutangaza ndoa ili mambo yaende vizuri. Kama unavyoniona nina kila kitu, sasa sioni sababu ya kunizuia kuoa,” alizungumza Tino kiasi cha kumfanya mama yake atabasamu.
Usiku ulipoanza kuliteka anga la dunia, Mama Tino alijikuta akizidiwa na usingizi uliotokana na uchovu mkubwa, akaingia chumbani kwake na kulala.
Tino wakati huo alitoka kwenye ua wa nyumba yake na kuketi huku akinywa juisi na kufurahia mafanikio yake. Simba hakuwa mbali bali alizungukazunguka karibu ya bosi wake na kutikisa mkia.
Mara kidogo alifika Jackline, Tino akaona ni muda sahihi wa kumwambia alichoongea na mama yake; Jackline alionekana kufurahia sana wazo hilo la kufunga ndoa.
Siku zilienda huku taratibu za ndoa nazo zikishamiri hasa kwanza kwa kuzikutanisha familia zote mbili kwa ajili ya hatua za awali.
Kila kitu kilienda sawa na wakawa wamebakiza mwezi mmoja tu kabla ya ndoa yao. Michango ilikuwa ikimiminika kila kona huku ndoa hiyo ikikaridiwa kuhudhuriwa na viongozi wakubwa wa serikali waliopewa mualiko.
Mahari ilitolewa kwa mujibu wa mila za Kichaga yaani upande wa bibi harusi mtarajiwa Jackline, kila gharama iliyotakiwa kulipwa kwa wakati huo, Tino alikuwa tayari ameshalipa.
 Lakini kadri siku zilivyozidi kukaribia ndipo Tino alishangaa kuona mkewe mtarajiwa akizidi kunenepa kiasi kwamba lile shela alilomnunulia siku chache nyuma likianza kumbana.
Alishangaa pia kumuona mchumba wake huyo akibadilika kila siku kitabia na kuanza wivu uliokithiri, hakujua ni nini.
Maudhi yalivyozidi alitamani hata ndoa hiyo aiharishe na kumtimua Jackline nyumbani kwake, lakini aliamua kumshirikisha mama yake kwanza.
Mama huyo mtu mzima aliyejua mambo mengi ya duniani alicheka na kumnong’oneza Tino; “nenda mkapime inawezekana amenasa ujauzito.”
Kweli walivyopima Jackline alionekana ana ujauzito wa wiki mbili. Wote wakajikuta wakifurahia na kumshukuru Mungu kwa kuwabariki zaidi.

ITAENDELEA JUMANNE


Post a Comment
Powered by Blogger.