MAKALA: WAGENI KARIBUNI, LAKINI MSIWE KERO KWA WATOTO

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


NI kwa familia zote za mijini na vijijini suala la kutembelewa na wageni ni la kawaida katika mahusiano ya kijamii.
Wageni wanaweza wakawa ndugu, jamaa, marafiki. Nyumba inayotembelewa na wengi pia huwa ni ishara ya upendo kwa upande mwingine na Kama Mzazi hilo mimi sina ubishi nalo. Lakini pia una hiari ya kukubaliana nami au la juu ya dhana kwamba wakati mwingine wageni wakija ndani ya familia huwa ni kero kwa watoto wa mwenye nyumba.
Hufikia hatua watoto wa mwenyeji kunyanyasika badala ya kuwa na furaha ya kupokea wageni. 
Hali huanzia pale ambapo chakula cha siku kikiwa hakitoshi au kwa bahati mbaya pale ambapo wageni wenyewe wakija bila taarifa yoyote kwa kigezo tu kwamba ninakwenda kwa kaka yangu, mdogo wangu au hata kwa mwanangu bila kutoa taarifa.
Labda kwa hili la taarifa sina budi kulisemea hususani kwa siku hizi kwani mawasiliano yamerahisishwa mno. Huwezi kudai kwamba ulikuwa huna namna ya kufanya mawasiliano kabla ya kwenda kumtembelea jamaa au ndugu yako. Siku hizi mawasiliano yapo kiganjani tu.
Hata kama huna simu yako binafsi, ujitahidi kumwomba jirani utume hata ujumbe kwamba nitakuja kwako tarehe fulani. Si vibaya pia kujua kama mwenyeji wako atakuwa na nafasi, kwa maana ya uwezo wa kukuhudumia siku hizo utakazokuwa mgeni wake. Hebu fikiria uko mjini na mgeni kaja nyumbani na watoto wawili, tena mmoja wa kike na mwingine wa kiume.
Mwenyeji wako amepanga chumba kimoja na sebule ambayo usiku hugeuka chumba kingine kwa watoto wake na wageni ndiyo hao watatu, wameingia, atafanyaje? Mila na desturi zetu za kiafrika na ukarimu tulionao hata katika hali ngumu kama hiyo, mwenyeji atajitahidi kuwakirimu wageni wake, atatafuta chakula hata kama itamlazimu kukopa.
Lakini kwa suala la malazi, waathirika mara nyingine kutokana na ujio wa wageni ni watoto. Ni vigumu kwa baba na mama kuhama ‘ikulu’ yao kupisha wageni hivyo kinachobakia hapo ni kuhamisha watoto na kuwaombea nafasi kwa majirani au wapangaji wenzao.
Wakati mwingine kutokana na mtindo huo wa kuwahamisha watoto kwenda kulala kwa jirani kupisha wageni ipo hatari ya watoto kujifunza tabia ambazo huenda zikaanza kuwaletea athari katika makuzi yao kwa sababu huwezi kujua pia tabia na mwenendo wa watoto wa jirani.
Kuna ugeni wa dharura, unaweza kuvumiliwa lakini unapokuwa siyo ugeni wa lazima ndio unakera sana. Mbaya zaidi kuna wageni ambao husafiri na masharti yao ama sheria zao. Mara sili hiki, siwezi kulala vile na mengine kama hayo na wengine hawasomi mazingira.
Unakuta ugeni wake si wa lazima, unasababisha adha kibao kama hizo za watoto kulala kwa jirani, lakini hana mpango wa kurejea kwake mapema iwezekanavyo. Hivi kwa nini tusiweze kubadilika kutokana na uhalisia wa maisha yalivyo hivi sasa?
Kwa nini tushindwe kutoa taarifa ili basi angalau mwenyeji aweze kujiandaa hata mahali pa kulala wageni wake na kuwasitiri watoto ambao ni jukumu lake la kwanza kwa kila mzazi makini?
Hebu fikiria kama kwa mwaka kutakuwapo na wageni wa aina hii ambao huja bila taarifa mara kama nne au sita hivi, je, utawalaumu watoto wa mwenyeji wakianza kuchukia wageni au hata kupata athari hasi kwa kuiga tabia mbaya?
Wazazi wenzangu hebu tujitahidi kurahisisha maisha ya wenyeji wetu kwa kuchukua hatua stahiki za kuarifu mapema, kusafiri na idadi ndogo ya watu ili tusiwe karaha kwa mwenyeji na angalau jitahidi kuleta pia chochote kwa familia unayoitembelea.
Kama umetokea kijijini, basi ulete mchele, mihogo, ndizi, maharage au mahindi na kwa wale wa mjini nenda kasalimie kijijini na mikate, sukari, nguo hata kama ni za mitumba na chochote kile ambacho unadhani ni anasa kijijini. Zawadi kama hizo zitakuweka karibu zaidi na mwenyeji wako na watoto nao watakukumbuka unapoondoka kurudi kwako.

nvikonko@gmail.com
 0766843382
Post a Comment
Powered by Blogger.