LEO KATIKA HISTORIA: ITAMBUE SIKU YA MTOTO WA AFRIKA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Katikati ya Juni mwaka 1976, vyombo vya habari sehemu nyingi duniani, vilipambwa na picha ambayo siyo rahisi kuisahau.
Picha hiyo ilimwonyesha mtoto wa shule nchini Afrika ya Kusini, aliyetapakaa damu akihangaika kukimbia huku akiwa amembeba mwenzake aliyekuwa akibubujikwa na damu.
Mwenzake huyo alikuwa ameshakufa baada ya kupigwa risasi na askari wa utawala wa Makaburu! Tukio hili la kusikitisha lilitokana na maandamano ya amani yaliyokuwa yakifanywa na watoto wa shule katika kitongoji cha Soweto, waliokuwa wakipinga elimu duni iliyokuwa ikitolewa kwao na utawala huo wa kibaguzi.
Katika vurugu hizo zilizodumu kwa wiki mbili, zaidi ya watoto mia moja wa shule waliuawa na maelfu wengine kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari hao wa Makaburu.
Ili kuwakumbuka watoto hao waliouawa kikatili, tangu mwaka 1991 nchi zote za Afrika, ikiwamo Tanzania, zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika ili kuhakikisha kuwa haki za watoto zinazingatiwa katika bara lote la Afrika.
Tanzania kama moja ya nchi za Kiafrika nayo imekuwa ikiiadhimisha siku hii, japo sijui kama Serikali inajua chanzo cha maadhimisho haya.
Enzi za Mwalimu Julius Nyerere, sekta ya elimu ilikuwa ikiongozwa na Sera ya Elimu ya Kujitegemea. Wakati huo, mhimili mkuu wa sera hii ilikuwa ni nia thabiti isiyo na chembe za unafiki ya uongozi wa nchi kuwapatia elimu bora watoto wote wa Tanzania.
Hii ilithibitishwa na ukweli kuwa mtoto wa mkulima maskini kutoka kijijini Kahama, Liwale au Muleba aliweza kusoma darasa moja na mtoto wa waziri. Ili kuhakikisha kuwa hili linafanyika kwa vitendo, Serikali ilibeba dhamana ya kulipia gharama za elimu ya watoto wote ili kuhakikisha kuwa Taifa linapata nguvu kazi iliyoelimika kwa kazi ya kulikomboa pamoja na wananchi wake.
Ni kutokana na ukweli huo ndiyo maana viongozi wetu wengi leo wako hapo walipo. Bila ya sera hii wengi wetu tusingeweza kufika hapa tulipo.
Sasa hivi elimu ya Tanzania, imewagawa watoto wa Kitanzania katika makundi mawili; kuna elimu ya watoto wa walalahoi na ile ya walio nacho.
Tofauti na enzi za Mwalimu Nyerere ambapo kulikuwa na nia ya dhati ya kutoa elimu bora kwa watoto wote wa Kitanzania, sasa elimu bora inapatikana katika shule za gharama kubwa ambazo ni watoto wa matajiri pekee ndiyo wanaomudu gharama hizo.
Shule hizi za gharama ndizo zenye mazingira mwafaka ya kufundishia na kujifunzia. Zina vifaa muhimu vya kufundishia, kama vile vitabu, maabara, maktaba na walimu wa kutosha.
Shule za aina hii kwa sasa ni zile za binafsi zinazotoza ada kubwa mno. Kiwango cha ada katika shule hizi kinazidi kiwango cha ada ya mwanafunzi wa shahada ya pili chuo kikuu!
Watoto wa walalahoi ambao ndiyo wengi hawana fursa hiyo tena. Hawa wamejengewa kiini macho cha elimu inayotolewa na taasisi zilizojengwa na kubatizwa jina la ‘shule za kata.’
Shule hizi hazina vifaa muhimu kama vitabu maabara, maktaba, vyoo wala walimu wa kutosha. Aidha, madarasa yamefurika, jambo linalowakandamiza watoto wa maskini wanaosoma kwenye shule hizo. Watoto wa Soweto walimwaga damu yao kupinga ubaguzi katika elimu. Elimu nchini Tanzania sasa inatolewa kwa misingi ya matabaka.
Tujiulize Tanzania inapoadhimisha Siku Mtoto wa Afrika huwa inafanya dhihaka?
Robert Mihayo ni Mratibu wa Ubora katika Shirika la HakiElimu. Anapatikana kwenye Simu namba 0755 319 308 na Emeli: media@hakielimu.org
Post a Comment
Powered by Blogger.