MZIMU WA ‘BUNGE LIVE’ WAMWANDAMA NAPE

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mzimu wa kuzuia shughuli za Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni uliopachikwa jina la ‘Bunge Live’, umeendelea kumwandama Waziri wa Habari, Nape Nnauye baada ya juzi kupokewa kwa kelele kiasi cha kushindwa kuhutubia wapenzi wa muziki jijini Mwanza.
Nape alitangaza uamuzi wa kusitisha kurusha moja kwa moja baadhi ya shughuli za Bunge, akisema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) linashindwa kumudu gharama, lakini wabunge, hasa kutoka vyama vya upinzani wamepinga hatua hiyo wakisema inawanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata habari kuhusu chombo chao cha kutunga sheria.
Lakini Serikali imeshikilia msimamo wake, ikitoa sababu tofauti na kwenda mbali zaidi kuzuia vituo binafsi vya televisheni kurusha matangazo, huku TBC1 ikirusha kipindi cha maswali na majibu pekee ikielezwa kuwa huo ni uamuzi uliopitishwa katika Bunge la 10.
Juzi, Nape aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha la Jembeka Festival lililofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, alipokewa na kelele za maneno “Bunge Live” wakati akikaribishwa kuhutubia mamia ya wapenzi wa burudani waliohudhuria tamasha hilo, ambalo lilijumuisha wasanii nyota kama Shaffer Chimere Smith a.k.a Ne-Yo kutoka Marekani na Diamond Platnum.
Baada ya mkurugenzi wa kampuni ya Jembe ni Jembe, Sebastian Ndege kumkaribisha waziri huyo kuzungumza na wananchi hao, Nape alisimama lakini akapokewa kwa kelele.
“Bunge live, Bunge live, Bunge live,” walipiga kelele mashabiki waliohudhuria tamasha hilo.
Kelele za “Bunge Live” zilisababisha Waziri Nape kushindwa kuhutubia na kulazimika kuketi chini na Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula alisimama kujaribu kuokoa jahazi, lakini naye akakumbana na kimbunga cha sauti za wananchi walioamua kulitaja jina la mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Ezekia Wenje.
“Wenje, Wenje, Wenje,” wananchi hao waliimba kwa sauti wakati Mabula akijaribu kuwatuliza ili Nape ahutubie.
Akizungumzia tukio hilo, Nape alisema wananchi waliompigia kelele za “Bunge Live” walisukumwa na masuala ya kisiasa, ndiyo maana aliepuka kuendelea kuzungumza ili kutochafua hali ya hewa uwanjani.
“Pale uwanjani tulikwenda kwa ajili ya burudani, sasa baada ya kuona wananchi wanaanza kuleta masuala ya kisiasa nikaona ni busara kuacha kuhutubia. kuepusha shari,” alisema Nape.
Pamoja na Nape, tamasha hilo pia lilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Mabula.
Ukiachilia mbali dosari hizo, tamasha hilo lilikonga nyoyo za wapenzi wa sanaa ya muziki waliokesha uwanjani hapo hadi saa 11:00 alfajiri wakiburudishwa na wasanii nguli.
Wasanii wengine waliopata nafasi ya kutumbuiza ni Juma Nature, Ney wa Mitego, Ruby na Fid Q.

Maoni ya wadau
Wadau waliozungumza na Mwananchi wameitaka Serikali kuangalia upya uamuzi wake baada ya tukio hilo la Mwanza.
“Unapotenda mambo lazima ukumbuke na historia,” alisema mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Kasaka ambaye alikumbusha kiini cha Serikali kuamua kuonyesha moja kwa moja shughuli za Bunge wakati wa utawala wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Rais Mkapa alikuwa na sera ya uwazi na ukweli. Kwa kuonyesha Bunge moja kwa moja ni kuweka uwazi kwa wananchi ili wajue nchi yao inakwendaje.”
Kasaka aliyewahi kuwa mbunge wa Lupa ambalo sasa lipo mkoa mpya wa Songwe, alisema kuonyesha Bunge moja kwa moja kunawasaidia wananchi kujua yupi ni kiongozi bora na yupi hafai.
“Hata kama nchi nyingine hazionyeshi live, kusitunyime sisi uhuru wa kuangalia Bunge letu. Kuna mtu amesema eti watu hawafanyi kazi, hiyo siyo kweli. Hizo TV walizoweka ofisini ni za nini?” alihoji Kasaka.
Mtaalamu wa masoko wa kampuni ya The Exchange, Lucas Moreto alisema kitendo cha kukatisha maonyesho ya Bunge ya moja kwa moja kimewanyima wananchi haki ya kupata habari.
“Ukilitazama suala hili kwa undani utaona kuwa wananachi wamebaki ndani ya sanduku, hawaelewi kinachoendelea nje. Nasikia kuna televisheni ya Bunge lakini bado wananchi hawapati haki ya kuangalia kinachoendelea wakati wote. Ni kuwanyima tu haki ya kupata habari,” alisema Moreto.
Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema hatua hiyo imetia doa Serikali ya Rais John Magufuli.
“Utawala wa Awamu ya Tano umejipambanua kuwa na malengo ya kupigania haki za wanyonge. Hata wanapotumbua majipu husema ni kwa ajili ya mamilioni wanaoteseka kwa kukosa huduma vijijni,” alisema na kuongeza:
“Sasa malengo hayo inabidi yajidhihirishe kila kona, ikiwamo kisiasa. Kuona Bunge live inachukuliwa kama nafasi ya wanyonge kutathmini utendaji wa wawakilishi wao. Hivyo basi, hatua hii ya kufuta Bunge live haitapokewa vizuri na inatia doa nia nzuri ya Serikali ya awamu hii.”

Nyongeza na Elias Msuya
Post a Comment
Powered by Blogger.