MAGARI YA WASHAWASHA KUGEUZWA YA ZIMAMOTO

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


aibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yusufu Hamad Masauni, amesema Serikali iko katika mchakato wa kuangalia uwezekano wa kubadili matumizi magari ya polisi ya kuzuia ghasia kwa kurusha maji ya kuwasha maarufu washawasha yaweze kutumika kuzima moto.

Kauli hiyo ilitokana na swali la nyongeza la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga aliyeuliza ni kwanini Serikali inanunua magari ya washawasha yasiyo na tija ambayo hutumika nyakati za uchaguzi tu badala ya kununua magari ya zimamoto.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Masauni alisema magari ya washawasha bado yana tija kwani Serikali inafanya taratibu ili magari hayo yatumike kuzima moto kwenye majanga na isiwe kwa washawasha pekee na kuwataka wabunge hasa wa upinzani kuondoa fikra za kuyapinga magari ya washawasha kwani sasa itakuwa ni neema kwao badala ya kutumika kwa kudhibiti vurugu pekee. 
Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana Serikali ilinunua magari ya washawasha 777 kwa bei ya kati ya Sh150 milioni na Sh400 milioni, hata hivyo taarifa zingine zilisema magari yaliyotumika wakati wa uchaguzi ni 50.

Awali Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka (Chadema), aliuliza swali la msingi kwamba ni lini Serikali itapeleka huduma ya zimamoto katika mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea.

Naibu Waziri Masauni alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika halmashauri ya Mji wa Tunduma lina kituo katika eneo la mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe, kinachohudumia wilaya yote ukiwamo mpaka huo.

Alisema kwa sasa kituo hicho kina gari moja ambalo nalo liko kwenye matengenezo mjini Mbeya likiendelea kufanya matengenezo huku askari wakiendelea kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na majanga ya moto.

Masauni alisema ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya zimamoto katika maeneo ya nchi ikiwamo Tunduma, mpango huo unategemea upatikanaji wa fedha kwa Serikali.

Kuhusu ujenzi wa kituo cha Polisi cha Mbozi, alimuomba mbunge wa eneo husika avute subira ili waweze kuona namna bora ya kufanya kwani bajeti ya Serikali ni ndogo na vituo vinavyotakiwa kujengwa ni vingi.
Post a Comment
Powered by Blogger.