RIPITI YA CAG YATAJA VINARA WA MADENI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Asaad  

Jeshi la Polisi limeibuka kinara miongoni mwa taasisi 91 za Serikali zilizolimbikiza madeni hadi kufikia Sh1.4 trilioni, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha.
Ripoti hiyo ya hesabu zinazoishia Juni 30, mwaka jana, inasema jeshi hilo linaongoza kwa kudaiwa Sh385 bilioni likifuatiwa kwa mbali na Wizara ya Afya inayodaiwa Sh180.8 bilioni.

Kauli ya CAG
CAG, Profesa Mussa Juma Asaad anasema: “Sehemu kubwa ya deni ni kutoka Jeshi la Polisi ambalo ni sawa na asilimia 27 ya jumla ya deni lote; ya pili ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwa na asilimia 13 na Wizara ya Maji asilimia 10 ya deni lote.”
CAG anasema jumla ya madeni hayo imeongezeka mara mbili kutoka Sh772.5 ya mwaka uliotangulia hadi Sh1.4 trilioni sasa. “Kumekuwapo na ongezeko kubwa la madeni kiasi cha Sh671,350,983,378.30 sawa na ongezeko la asilimia 89,” anasema CAG katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni.
“Mwenendo wa deni, kwa kipindi cha miaka miwili, utaathiri utekelezaji wa mipango ya Serikali. Hii ni kwa sababu, badala ya kutekeleza mipango iliyopo, itakuwa inalipa madeni ya miaka ya nyuma,” inasema taarifa hiyo.
CAG anaongeza kuwa ongezeko kubwa la deni bila ya kuonyesha juhudi za kulilipa linavuruga uhusiano mzuri uliokuwapo kati ya wizara, wakala, idara na sekretarieti za mikoa pamoja na watoa huduma wake na watumishi; na huweza kusababisha utoaji wa huduma usioridhisha kwa umma.”
Anasema taasisi hizo zinaweza kushtakiwa kwa kosa la kushindwa kulipa deni kwa wakati hivyo: “Ninapendekeza kwa Serikali kuhakikisha fedha zinatolewa kama zilivyoidhinishwa na kupitishwa na Bunge ili kupunguza limbikizo kubwa la deni ambalo linaweza kusababisha hatari ya kudaiwa na kupunguza uaminifu, kuingiza katika bajeti ya mwaka ufuatao madeni yote ili kuepuka mgogoro na watoa huduma na wadau wengine.”
Pia, anaitaka Serikali kupitia upya mchakato wa maandalizi ya bajeti ili kuhakikisha ile inayoandaliwa inaendana na shughuli zilizopangwa na mahitaji yote kwa ujumla.

Kitwanga asema hajui
Alipoulizwa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hafahamu lolote na hawezi kuzungumzia suala hilo badala yake aulizwe Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira ambaye hata hivyo, hakupatikana alipopigiwa simu.
“... Hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa, mtafute Katibu Mkuu atakupa majibu,” alisema Waziri Kitwanga.

Ummy na deni la MSD
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kwa sasa watahakikisha wanapata fedha kutoka Hazina ili kumaliza madeni hayo hasa yale ambayo ni ya mikataba ya huduma zilizokwishatolewa.
“Mfano deni la MSD la zaidi ya Sh120 bilioni ambalo kati yake Sh67 bilioni zimehakikiwa na CAG, tumetenga fedha katika bajeti ijayo kulilipa,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali sasa imefuta huduma ya chakula kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya Serikali vya uuguzi na utabibu, hivyo wanafunzi wanatakiwa kujigharamia.
Kuhusu wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi, alisema Serikali itawapunguza na kujenga uwezo kwa hospitali za ndani.
“Hivi sasa deni ni zaidi ya Sh28 bilioni, hivyo tumedhamiria kujikita katika kujenga uwezo wa ndani kwa kusimika vifaatiba vya kisasa,” alisema.
Simbachawene: Sababu ni siasa
Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema madeni hayo yanatokana na mashinikizo ya kisiasa ya kutaka fedha zilizopangwa kufanya miradi mbalimbali kuhamishiwa katika matumizi mengine.
“Mfano, hili suala la Katiba Mpya, kuna fedha zilitengwa kwa ajili ya shughuli nyingine katika halmashauri lakini kutokana na wapinzani kushinikiza Katiba Mpya wakati mtizamo ulikuwa kuirekebisha iliyopo, baadhi ya fedha zilipelekwa kwenye mchakato wa kuipata Katiba hiyo,” alisema Simbachawene.
Alisema zipo fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya matumizi muhimu katika halmashauri lakini zilipelekwa katika Uchaguzi Mkuu kwa sababu tu ya mashinikizo ya kisiasa ambayo wakati mwingine yanakuwa hayana msingi.

Dk Mahiga anatafiti
Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema bado anawasiliana na wataalamu wake kujua sababu ya kuwapo kwa deni hilo katika wizara yake.
“Jana tu nimewaagiza wataalamu wangu waniletee taarifa ya madeni ya wizara, nadhani tuwasiliane kuanzia kesho nitaweza kueleza mikakati ya kulipa. Ni kweli tumepata hati safi ya CAG, lakini hayo madeni bado sijayajua,” alisema Dk Mahiga.

Taasisi nyingine
Taasisi iliyoshika nafasi ya tatu kwa madeni ni Wizara ya Maji inayodaiwa Sh150.5 bilioni ikifuatiwa na Wizara ya Ujenzi (Sh135.7 bilioni), Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) inayodaiwa Sh93.2 bilioni na Jeshi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ (Sh91.5 bilioni).
Nyingine ni Jeshi la Kujenga Taifa – JKT (Sh67.9 bilioni), Jeshi la Magereza (Sh59.2 bilioni) Hazina (Sh38.5 bilioni) na nafasi ya 10 imechukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje inayodaiwa Sh21.1 bilioni.
Taasisi yenye madeni kidogo iliyoshika nafasi ya 91 katika orodha hiyo ni Ubalozi wa Tanzania, Lilongwe, Malawi unaodaiwa Sh14, 292,697.

Vielelezo vya deni
Katika ripoti yake, CAG amefichua kuwapo kwa taasisi tatu za Serikali ambazo hazikuonyesha viambatanisho vya malipo yanayofikia Sh23.3 bilioni yanayotokana na huduma kutoka kwa wazabuni mbalimbali.
“Taasisi husika zilishindwa kuthibitisha uhalali wa madai hayo baada ya kushindwa kuwasilisha viambatisho na nyaraka za uhalali wake. Maofisa masuuli wanaohusika waweke mifumo ya udhibiti iliyo madhubuti ili kuhakikisha madai yote kwenye taarifa ya fedha yanakuwa na nyaraka zinazothibitisha huduma iliyotolewa,” anasema.
Taasisi hizo ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Sh3.2 bilioni), Wizara ya Mambo ya Ndani (Sh1.8 bilioni) na Wizara ya Afya (Sh18.3 bilioni).
Post a Comment
Powered by Blogger.