UPDATES:KAMPUNI YA RIFARO YADAIWA KUTOKUWA NA LESENI YA TCRA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
ISO 9001:2008 CERTIFIED

TAARIFA KWA UMMA


KUTUMIKA RASILIMALI NAMBA MAALUMU 15420 NA KAMPUNI YA RIFARO BILA CHETI CHA MATUMIZI YA NAMBA CHA MAMLAKA YA MAWASILIANO


1.0   UTANGULIZI
1.1. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia huduma za Sekta ya Mawasiliano na Utangazaji nchini, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa rasilimali namba kwa mawasiliano na anwani kuhakikisha matumizi sahihi.

1.2. Katika siku za hivi karibuni, Mamlaka imeona taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu Kampuni ya RIFARO AFRICA LIMITED kuwa na leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano. Yafuatayo ni maelezo ya Mamlaka kuhusu taarifa hizo:

1.3.Mnamo tarehe 28 Julai, 2014 Mamlaka ilitoa kwa RIFARO AFRICA LIMITED Cheti cha Matumizi ya Rasilimali Masafa kwa ajili ya huduma za ziada za Mawasiliano kupitia SMS (VAS SMS CODE) namba maalumu 15420 kutumika katika kutengeneza mfumo wa Mawasiliano wa SMS kuunganisha na kupokea taarifa za mawakala wao wa kuuza na kusambaza muda wa maongezi kupitia wavuti yao (website);

1.4.Mnamo tarehe 27 Julai, 2015 Cheti hicho kilimalizika muda wake na Kampuni ya RIFARO Africa Limited haikuomba kuongeza muda wa matumizi wa rasilimali namba maalumu 15420. Kuendelea kutumia rasilimali namba hiyo bila cheti cha kuruhusu kufanya hivyo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano ni ukiukwaji wa Kanuni ya 17 (1) ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 - Matumizi ya Namba na Anwani za Mawasiliano - (Electronic Communication Numbering and Addressing) Regulations, 2011.

2.0   AMRI YA UTEKELEZAJI


Mnamo tarehe 24th Februari, 2016, Mamlaka ilitoa Amri ya Utekelezaji kwa kampuni ya RIFARO AFRICA LIMITED kwa mujibu wa Kifungu cha 45 cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania sura ya 172 kama ilivyorekebishwa na Kifungu cha 179 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielectroniki na Posta, na kuimauru kampuni hiyo kufika mbele ya Mamlaka ya Mawasiliano kujitetea kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kuvunja na kukiuka Kanuni namba 17 (1) ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya Mwaka 2011 - Matumizi ya Namba na Anwani za Mawasiliano kwa kutumia rasilimali namba maalumu 15420 bila Cheti cha kuruhusu matumizi yake kutoka Mamlaka ya Mawasiliano.

3.0 KUSIKILIZA SHAURI

Katika kusikiliza shauri la utetezi wa RIFARO AFRICA LIMITED:

1. Walikubali kupewa kibali cha kutumia rasilimali namba maalumu 15420 na kukubali pia kuwa matumizi yake yaliisha muda wake mwezi Julai, 2015;
2. Aidha walikubali kuwa Cheti Cha Matumizi ya Rasilimali Namba Maalumu 15420 kilipokwisha muda wake hawakuomba kuongezewa muda wa matumizi yake;
3. Hali kadhalika walikiri wameingia mkataba wa kibiashara na Kampuni ya Zanzibar Telecom Limited (ZANTEL) kwa ajili ya huduma ya Ezzy Pesa kama mtoa huduma mkubwa wa kampuni hiyo (mobile money super dealership).

4.0 MAAMUZI YA MAMLAKA

RIFARO AFRICA LIMITED imekuwa ikitumia rasilimali namba maalumu (VAS SMS CODE) 15420 bila cheti cha Mamlaka kuwaruhusu kufanya hivyo kinyume na Kanuni ya 17 ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2011 (Electronic Communication Numbering and Addressing) Regulations, 2011.

Baada ya kutafakari utetezi wa Kampuni ya RIFARO AFRICA LIMITED na matokeo ya utetezo wao, Mamlaka inatoa maamuzi kama ifuatavyo:

1. RIFARO AFRICA LIMITED kulipa kwa Mamlaka faini ya shilingi milioni 10 (TZS 10,000,000) kwa kutumia rasilimali namba maalumu 15420 bila cheti cha kuruhusu kufanya hivyo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano; na

2. RIFARO AFRICA LIMITED iache mara moja kutumia rasilimali namba maalumu 15420 kwa kuwa haina ruhusa ya kufanya hivyo kutoka Mamlaka ya Mawasiliano.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inapenda kuarifu umma kuwa RIFARO AFRICA Limited haina leseni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Kampuni hii ilikuwa na Cheti cha matumizi ya rasilimali namba maalumu 15420 ambacho kiliisha muda wake tangu mwezi Julai 2015.

Dkt. Ally Y. Simba
MKURUGEZI MKUU

02/03/2016


Post a Comment
Powered by Blogger.