UPDATES: WANNE WAFARIKI NA 38 WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI ILIYOTOKEA USIKU WA KUAMKIA LEO MKOANI IRINGA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Harakati za kutoa miili ya marehemu zikiendelea

Watu wanne wamefariki papo hapo na wengine 38 wakijeruhiwa vibaya ikiwa ni pamoja na kukatika viungo, kufuatia ajali ya basi iliyotokea majira ya saa tano usiku wa leo mjini Iringa. Basi hilo lenye namba za usajili T 798 AKV mali ya kampuni ya Lupondije Express lilikuwa likitokea mjini Mwanza kuelekea mjini Iringa.
Taarifa ambazo mwandishi wa habari hizi amezipata toka eneo la tukio, zinabainisha kuwa, chanzo cha ajali hiyo, ni kufeli kwa mfumo mzima wa breki, ambapo gari hilo likiwa katika mteremko mkali wa Ipogoro, lilimshinda dereva na kugonga kingo za barabara na hatimaye kuanguka.

Inaelezwa kuwa, basi hilo ambalo lilikuwa limalizie safari yake katika stendi kuu ya mjini Iringa, lililazimika kwenda stendi ndogo ya Ipogoro, ili kufaulisha abiria waliokuwa wakielekea Mbeya, kwenye basi la Hood lililokuwa likitokea Arusha.
Taarifa zaidi zinafafanua kuwa, dereva wa basi hilo, awali aliingia kwenye mzozo na abiria waliokuwa wakiishia Iringa, kufuatia kutokuingia stendi kuu kuwashusha, ambapo aliwaambia kwamba anaenda kwanza kufaulisha abiria waliokuwa wakiendelea na safari ndio arudi kuwashusha waliokuwa wamefika.
Na ni kama abiria hao walikuwa wanajua kuwa huko mbele si salama, kwani takriban kilomita mbili mbele, ndio wakakumbana na mkasa huo wa kusikitisha.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa eneo la tukio muda mfupi baada ya kutokea kwake, ameshuhudia miili minne ikitolewa, katika basi hilo, ambapo mwili wa mwisho kutolewa pamoja na mkono wa mmoja wa marehemu vilikuwa vimenasa kiasi cha kulazimika kutumia gesi kukata sehemu ya basi hilo ili kuweza kuvitoa.
Miili ya wanaume wawili inasemekana kuwa ni ya wakazi wa hapa hapa Iringa mjini, huku miwili iliyosalia ambayo ni ya wanawake, ikiwa haijatambuliwa.
Miili hiyo ikehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa ww Iringa, ambako pia majeruhi wa ajali hiyo wamefikishwa kupatiwa matibabu.
Hadi taarifa hii inachapwa, katika eneo la tukio, kamanda wa kikosi cha askari wa usalama barabarani (RTO) Leopard Fungu, alikuwa akiendelea kusimamia ziezi la kujaribu kulinyanyua basi hilo ili kuweza kukusanya baadhi ya mizigo iliyokuwa kwenye gari hilo.
Hata hivyo, zoezi hilo lilikuwa linaleta shida kutokana na ukosefu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na gari lenye uwezo wa kunyanyua basi hilo, ingaww juhudi za kupata nguvu toka kwa wasamaria zilikuwa zikifanywa.
Katika eneo la tukio, pia walikuwepo mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesera, mkuu wa mkoa, Amina Masenza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa.
Post a Comment
Powered by Blogger.