LEO KATIKA HISTORIA: MTAMBUE RAIS MAGUFULI ALIPOTOKA MPAKA SASA ALIPO

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Rais John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 huko wilayani Chato Mkoani Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya mkoa mpya wa Geita) na mpaka sasa anamiaka 56.
Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, Biharamulo ambako alisoma kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 - 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Halafu alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu; hii ilikuwa mwaka 1981 – 1982.
Alipopata stashahada yake, moja kwa moja alikwenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati. Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983.
Kisha alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai hadi Desemba 1983), kisha akaenda kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi hadi Juni 1984).

Dkt.Abel Minani, Dkt.John P.J Magufuli na Dkt.John Kyaruzi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam muhula wa mwaka 1985/1986.
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.
Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Rais Dk Magufuli ana mke, watoto na familia imara.

MBIO ZA UBUNGE
Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.
Mwaka 2005 aliendelea kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge kwa kipindi cha tatu. Akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Lakini safari hii, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi mpaka anachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MBIO ZA URAIS
Dk Magufuli ni mmoja wa wana CCM ambao walikuwa wakitajwa sana kuwa anaweza kuwa mgombea sahihi wa CCM baada ya kipindi cha Rais Kikwete kumalizika. Lakini yeye mwenyewe alikuwa akikana na kutotaka kuhusishwa na kinyang’anyiro hicho. Hata hivyo, watu wa karibu na Dk Magufuli walisema kuwa aliwahi kufuatwa na vigogo wakubwa ndani ya CCM wakimwomba, wakati ukifika, achukue fomu. Yeye alikuwa na msimamo kuwa anapaswa kupima hali ya mambo kabla hajaamua kujihusisha na urais au la.

Tarehe 12 Julai 2015 alichaguliwa kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi na mgombea mwenza ni Samia Suluhu Hassani.  Dkt. John Magufuli aliwashinda wagombea wenzake kwa asilimia 87 % ya kura za wajumbe, hiyo ikiwa ni kura 2104. Daktari John Magufuli, aliwashinda wapinzani wake Bi Amina Salulm Ali na dakta Asha-Rose Migiro. 

Tarehe 29 Oktoba 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ulimtangaza kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wa kura 8,882,935 sawa na 58.46% pamoja na makamu wa rais Samia Suluhu Hassani huku mpinzani wake wa karibu Waziri mkuu mstaafu Mh. Edward Lowassa wa chama cha Chadema kupitia mwamvuli wa UKAWA akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.
Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa kama rais wa tano wa Tanzania, ingawa upinzani haujakubali matokeo hayo hadi leo.

UTEUZI WA WAZIRI MKUU NA MAWAZIRI
Tarehe 19 Novemba 2015 Rais Dr. John Pombe alipeleka pendekezo la jina la waziri mkuu kwa awamu ya Tano anayoiongoza. Rais alipendekeza Majaliwa Kassim Majaliwa kuwa waziri mkuu ambae alihitajika kuthibitishwa na bunge kwa kura za siri kabla ya kutangazwa rasmi. Alithibitishwa na bunge baada kupata kura nyingi zaidi za ndio hivyo kuwa waziri mkuu wa awamu ya tano. Wabunge 394 Wabunge waliosajiliwa 369 Wabunge wanaotakiwa kufika akidi 184 Wabunge waliopo na kupiga kura 351 Kura zilizoharibika 2 (0.06%) Kura za Hapana 91 (25.9%) Kura za Ndio 258 (73.5%). Tarehe 10 Desemba 2015 alitangaza baraza la mawaziri likiwa na watu 34 tu katika nafasi ya waziri na naibu waziri.

UWAJIBIKAJI WA SERIKALI YA MAGUFULI
Hakuna shaka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imevutia wengi katika muda wa takribani miezi minne ambayo imekuwa madarakani. Watanzania wengi wamekuwa na imani kubwa na Serikali ya Rais John Magufuli, baada ya kuanza kazi kwa kishindo huku ikifanya mambo ambayo huko nyuma ilionekana kwamba yana ugumu kufanyika.
Chini ya Rais Magufuli na kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu,’ Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha kwa vitendo, kupambana na maovu hususani ubadhirifu, wizi, uzembe na njama za kuhujumu mapato ambapo wakati wa kuzindua Bunge la Kumi na Moja, Dk Magufuli, alifananisha mapambano hayo na utumbuaji wa majipu.
Alifafanua kwamba ingawa majipu yanauma, lakini njia sahihi ya kuyaponesha ni kuyatumbua. Tangu waanze kazi hiyo ya kurejesha maadili katika utumishi wa umma, wananchi wameridhishwa na kazi hiyo ya viongozi wa Serikali ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli na msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye sasa huko mitaani anajulikana kama ‘Mzee wa Kutumbua Majipu’ au ‘Mzee wa Bandari.’
Wananchi wanafurahiswa jinsi Rais Magufuli na timu yake wanavyofanyakazi ya kurudisha nidhamu kwa watumishi wa umma bila kumuonea haya mtu yeyote. Ndiyo maana kwa watumishi wa umma sasa kila mmoja yuko roho juu anaposikia Waziri Mkuu, Majaliwa anatembelea eneo lao la kazi, kiasi wengine kueleza kuwa ni heri kukutana na Rais Magufuli kuliko Majaliwa.

IMEANDALIWA NA GEOFREY ADROPH WA PAMOJA BLOG

SOURCE: TOVUTI YA IKULU NA JULIUS MTATIRO

Kwa ufafanuzi zaidi msikose kutuandikia kupitia pamojapure@gmail.com
Post a Comment
Powered by Blogger.