LEO KATIKA HISTORIA: MTAMBUE HAYATI LUTENI JENERALI MAYUNGA NA VITA VYA KAGERA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.Hayati Luteni Jenerali Silas Peter Mayunga alizaliwa Maswa, Shinyanga mwaka 1940 na kufariki 2011 katika Hospitali ya Apollo, mjini New Delhi, India. Alijiunga na Jeshi la Tanganyika Rifles Januari 10, mwaka 1963, baada ya kumaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Bwiru, Mwanza. Alihitimu kozi ya Uofisa wa Jeshi Julai 26, 1963, nchini Israel, akahitimu kozi ya Unadhimu na Ukamanda wa Jeshi mwaka 1973 nchini Canada na kuhitimu kozi ya Ukamanda wa Juu wa Jeshi mwaka 1974 hapa nchini.

Itakumbukwa Novemba mosi, 1978, majeshi ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin yalivamia Mkoa wa Kagera. Uvamizi huo ulimsukuma Mwalimu Nyerere kuashiria ushindi kabla vita kuanza.Nyerere aliashiria ushindi kabla vita kuanza akisema; "sababu ya kumpiga tunayo, nia ya kumpiga tunayo na uwezo wa kumpiga tunao." Hakika, kauli hii ilihitaji si tu risasi za kutosha, mizinga au makombora na silaha za kila aina kuisimamia, bali mashujaa wa mstari wa mbele vitani.
Miongoni mwa wapiganaji waliotwikwa dhima hiyo nzito ni pamoja na Luteni Jenerali Silas Mayunga, sambamba na wapiganaji wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Watanzania kwa ujumla, waliotoa ng'ombe hata kuku kulisha wapiganaji uwanja wa mapambano.

Mstari wa mbele katika uwanja wa vita, Luteni Jenerali Silas Mayunga na wenzake, kazi ilikuwa moja tu-kufa au kupona ili kulinda si tu hadhi ya Tanzania, heshima ya wapenda haki duniani.


Ni vita hii ya Kagera ndiyo inayotajwa kumtambulisha zaidi Luteni Jenerali Mayunga ndani ya JWTZ na Jeshi la Uganda. Vita hiyo ilimpambanua ni mpiganaji wa aina gani akiwa mstari wa mbele.

Juni 21, mwaka 1995, ni siku ambayo Mayunga alijiwekea rekodi binafsi ya kushika cheo cha juu jeshini, akipandishwa cheo kuwa Luteni Jenerali na miezi sita baadaye (Desemba 31, 1995) alistaafu.
Mti mkavu akiwa jeshini

Mayunga ni kamanda kiongozi. Amekuwa Mkurugenzi wa Mafunzo makao makuu ya jeshi, Kamanda wa Brigedi ya 202 ya Tabora, na Kamanda wa Divisheni za 20 na 30 za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Huwezi kuzungumzia Operesheni Chakaza wakati wa vita dhidi ya majeshi ya Idi Amin bila kumtaja kiongozi wa operesheni hiyo ambaye ni Luteni Jenerali Mayunga.

Katika Operesheni Chakaza, Mayunga ndiye aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya 206. Ndani ya Jeshi la Uganda Mayunga ana historia muhimu. Amekuwa Kamanda wa Kikosi Maalumu cha JWTZ nchini Uganda kati ya 1979 na 1980.

Lakini ukiondoa pilikapilika za kijeshi, Mayunga amekuwa Mkuu wa Mkoa Singida mwaka 1977 hadi 1978, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria mwaka 1989 hadi 1998 na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) 1998 na 2002, alipostaafu.

Mungu aipe pumziko la amani nafsi yake na amlaze pema peponi hayati Mayunga 


Post a Comment
Powered by Blogger.