BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU YATOA ILANI MIKOPO KWA KIDATO CHA SITA

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa
 
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya vyuo vikuu mwaka huu wanatakiwa kutuma maombi yao ya kupata mikopo kabla ya Juni 30, mwaka huu bila kusubiri matokeo ya kidato cha sita.

Bodi hiyo imesisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza baada ya kipindi hicho huku ikiwashauri kutuma maombi yao kwa kutumia alama za matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.


Hayo yalisemwa na  Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, wakati akizungumza na NIPASHE kutoa ufafanuzi juu ya mwisho wa kutuma maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya vyuo vikuu nchini kwa ajili ya mwaka ujao wa masomo.


NIPASHE lilitaka kupata ufafanuzi kutoka HESLB baada ya baadhi ya wanafunzi waliohitimu kidato  cha sita mwaka huu kuhofia kukosa mikopo kutokana na matokeo ya mtihani kuchelewa kutolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).


Kwa kawaida, matokeo ya kidato cha sita hutolewa na Necta Aprili kila mwaka na baadaye Mei wanafunzi wenye sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu huanza mchakato wa kuomba mikopo HESLB kwa kutumia matokeo ya kidato cha sita.


Necta hadi sasa haijatangaza matokeo ya kidato cha sita kutokana na serikali kufuta matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na kuliagiza Necta kupanga madaraja upya baada ya kubainika kuwa ulitumika utaratibu mpya wa alama za ufaulu bila kushirikisha wadau na kusababisha asilimia 60 ya wanafunzi kufeli.


Kwa sasa Necta inatekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri ya kuyapamga upya matokeo hayo kabla ya kutangaza matokeo ya kidato cha sita.


Mwaisobwa alifafanua kuwa wanafunzi wanatakiwa kutuma maombi kwa kutumia matokeo ya kidato cha nne na nyaraka zingine muhimu zinazohitajiwa na HESLB.


Alisema HESLB itapata matokeo ya kidato cha sita moja kwa moja kutoka Necta pindi yatakapotoka huku akisisitiza kwamba wahitimu hao wa kidato cha sita watume maombi yao haraka katika muda uliopangwa.


“Sisi hatuhitaji matokeo ya form six (kidato cha sita), hata matokeo yakitoka leo, vyeti haviwezi kutoka leo leo, lazima vitachukua muda, hivyo nawasihi wanafunzi watume maombi ya mikopo kwa kutumia matokeo ya kidato cha nne,” alisema Mwaisobwa.


Alisema kuwa matokeo ya kidato cha sita yanaweza kuchelewa kutoka kutokana na matokeo ya kidato cha nne kufutwa na kusisitiza kuwa mwanafunzi bado ana nafasi ya kuomba mkopo kwa kutumia matokeo ya  kidato cha nne bila kumuathiri.


Mwaisobwa alisema ni vyema wanafunzi wakaanza kuomba mikopo sasa badala ya kusubiri siku ya mwisho ambayo alisema kuwa inaweza kuwasababishia usumbufu.


Alisema wanafunzi wanatabia ya kusubiri hadi siku ya mwisho ya maombi na kusababisha tovuti ya HESLB kuelemewa na mtandao kutokana na kila mwanafunzi kuifungua tovuti hiyo ili kuhakikisha anawahi kutuma maombi yake kabla muda haujamalizika.


Mwaisobwa alisema kuwa mwaka jana jumla ya wanafunzi 97,702 walipata mkopo kutoka HESLB katika bajeti iliyotengwa na serikali ya Sh. bilioni 345.

 
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment
Powered by Blogger.